Waziri wa viwanda Mhe Innocent Bashungwa akisalimiana na wananchi wa Kidabaga Kilolo mkoani Iringa leo baada ya kufanya ziara katika kiwanda cha chai kidabaga kilichofungwa kwa zaidi ya miaka 20 sasa
Waziri Bashungwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kidabaga Wilaya ya Kilolo
Waziri Bashungwa akiwa na viongozi mbali mbali wa Kilolo 
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kilolo Kilian Myenzi akitoa salamu za chama 

Mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto akionesha shamba la chai isiyochumwa 
Waziri wa  Viwanda na Biashara wa Mhe. Innocent Bashungwa amewataka wakulima wa zao la chai wilaya ya Kilolo mkoani Iringa kujiandaa na jitihada za serikali za kufufua kiwanda cha chai Kidabaga kilichoanzishwa na kufa bila kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 20 sasa .

Akizungumza leo  baada ya ziara yake ya kukagua miundo mbinu ya kiwanda hicho waziri huyo alisema lengo la serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Magufuli ni kuona viwanda zaidi vinaanzishwa na vile vilivyokufa vinafufuliwa ili kusaidia ukuzaji wa uchumi wa wananchi na Taifa .

Waziri huyo alisema amelazimika kufika wilaya ya Kilolo kukagua kiwanda hicho na kuanza mchakato wa kufufua kiwanda hicho baada ya kilio cha wananchi wakulima wa Chai wilaya ya Kilolo kilichotolewa bungeni na Mbunge wao Venance Mwamoto .

Hivyo alisema kuwa lazima wananchi wawe na imani na serikali yao na kuwa na uhakika kuwa kiwanda hicho lazima kifufuliwe na kuanza kazi ili kuwezesha wananchi wanaolima chai kuuza mazao yao karibu na kiwanda .

Alisema tayari mwekezaji wa kujenga upya kiwanda hicho alipatikana  ila kuna changamoto ndogo ndogo kutoka mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) changamoto ambazo watakaa na kuzifanyia kazi ili mwekezaji huyo kampuni ya DL Group ya Kenya .

"Lazima utata uliopo wa mwekezaji kuanza ujenzi wa kiwanda kumalizwa hata kama anadaiwa  kwa pamoja tukae chini ili kuangalia namna ya mwekezaji atakavyolipa ili kiwanda kijengwe na mwekezaji kulipa kodi anayodaiwa "

Kuwa ili kukabiliana na changamoto ya uanzishwaji wa kiwanda hicho lazima changamoto hizo zifanyiwe kazi ili ikiwezekana hadi mwezi ujao kukawa na majibu ya matumaini kwa wananchi ya kuanza kwa kiwanda hicho .

Waziri Bashungwa alisema kati ya vitu ambavyo serikali ya awamu ya tano haitaki kusikia ni kauli za mchakato kauli ambazo hazitoi mwelekeo wa matumaini ya watanzania kwa kile wanacho hitaji .

Hata hivyo alisema jitihada kubwa zimekuwa zikifanyika na wizara ya kilimo kuona kasi ya uzalishaji wa zao la chai nchini inaongezeka hivyo njia pekee ya kuendana na kasi hiyo lazima wizara ya viwanda kujenga viwanda vya kuwezesha mazao hayo kwenda kiwandani kisha sokoni. 

Hivyo alisema katika ziara yake hiyo amepata kuongoza na timu ya wataalam mbali mbali ili kuona mkwamo uliokuwepo wa kufufua kiwanda hicho na vingine unafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo .

Aidha alisema  kwa sasa mnada wa zao la chai unafanyika nchini Kenya ila serikali ipo kwenye harakati za kuanzisha mnada wa zao la chai katika bandari ya Dar es Salaam ili kuweza kuhahizisha soko zaidi kwa wakulima wa zao la chai nchini .

Katika hatua nyingine waziri Bashungwa alipongeza jitihada mbali mbali zinazofanywa na Mbunge wa Kilolo Mwamoto katika kuwapigania wananchi wakulima wa chai Kilolo na kuwa wananchi waendelee kuwa na imani na Mbunge wao pamoja na serikali ya CCM chini ya Rais Dkt John Magufuli .

"Natambua kipindi hiki ni cha kuelekea uchaguzi mkuu na wapo ngedere wachache ambao wanajipitisha kutaka ubunge  ila nawaelezeni wananchi Kilolo Mbunge wenu anawapigania sana acheneni na ngedere wanaotaka kuvuna bila kupanda  kila mmoja awafukuze ili kulinda mazao yetu "

Pia waziri Bashungwa amemtaka mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Kilolo Kiliani Myenzi kufanya kazi ya kuelimisha wananchi juu ya miradi mikubwa ambayo Rais Dkt Magufuli anafanya badala ya mwenyekiti huyo kuungana na wananchi wasiojua faida ya miradi hiyo kubeza.

Kauli hiyo aliitoa baada ya mwenyekiti huyo wa CCM wilaya ya Kilolo wakati akimshukuru waziri  huyo kudai kuwa miradi ya Reli ,ununuzi wa Ndege na mingine inayotekelezwa wananchi wa Kilolo haiwanufaishi wao wanataka kiwanda cha Chai tu .

Mbunge wa Kilolo Mwamoto aliwahakikishia wananchi wakulima wa chai Kilolo kuwa serikali inaendelea kuboresha miundo mbinu ya barabara ili wakulima kuweza kufikisha mazao yao kwa wakati sokoni.

Mwamoto alisema kuwa kuanza kazi kwa kiwanda hicho ni Ukombozi mkubwa kwa wakulima kwani kiwanda kina mashamba yenye ukubwa wa hekta 3600 ambazo sasa zimegeuka kuwa misitu mikubwa .

Huku mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdallah alimweleza waziri huyo kuwa kumekuwepo na mikakati mbali mbali ya kufufua kiwanda hicho chini ya uongozi wa wilaya na mkoa wa Iringa .

Alisema ili kukabiliana na changamoto ya uanzishwaji kiwanda hicho wilaya chini ya usimamizi wa ofisi ya mkuu wa mkoa ilishirikiana na benki ya Kilimo Tanzania (TADB) kutafuta mwekezaji ambapo juhudi ya wawekezaji watatu walijitokeza na kuonesha nia kabla ya kupatikana mmoja wa kampuni ya DL Group .
Akishukuru kwa niaba ya wananchi wenzake kwa ziara ya waziri huyo John Ndesekwa alisema wanamatumaini makubwa ya ziara hiyo kuleta matumaini ya kiwanda kufufuliwa
Share To:

Francis Godwin Mzee wa matukiodaima

Post A Comment: