Saturday, 4 January 2020

MBUNGE MASELE KUSAIDIA UJENZI WA ZAHANATI BUSHUSHU

Mbunge wa Masele mwenye suti nyeupe akiwa na viongozi wa jimbo CCM  akikagua ujenzi wa zahanati
.........................................................................
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Stephen Julius Masele (CCM) ametembelea na kukagua ujenzi wa zahanati ya Bushushu iliyopo katika kata ya Lubaga katika Manispaa ya Shinyanga na kuahidi kupeleka moramu na kutafuta fedha ili kukamilisha ujenzi huo ambao umefikia hatua ya renta.

Masele amefika katika zahanati ya Bushushu leo Ijumaa Januari 3,2020 ikiwa ni mwendelezo wa ziara  katika Jimbo lake kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wajumbe wa kamati za siasa CCM ngazi ya matawi na kata.

“Nimeridhishwa na kasi ya ujenzi wa zahanati ya Bushushu yenye vyumba 15 ambayo mimi mwenyewe niliuanzisha kwa kwa kuchangia mifuko 100 ya saruji.Niwapongeze sana wananchi na wadau mbalimbali kwa ushirikiano wenu kushiriki ujenzi wa zahanati hii.

“Nimerudi tena kwa mara pili kuwaunga mkono wananchi ili tukamilishe ujenzi huu na wananchi waanze kupata huduma za afya. Nitaleta moramu kujaza jengo hili pamoja na kutafuta fedha lakini pia nitazungumza na Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ili amalizie ujenzi kwa kupaua jengo hili kwani sisi wananchi tumeshajenga boma. Kwa utaratibu uliopo wananchi wakijenga boma,serikali inatakiwa kumalizia ujenzi”,alieleza Masele.

Mbunge huyo alisema serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya barabara,maji na umeme akibainisha kuwa huwezi kuzungumzia maendeleo ya mji wowote bila kugusa miradi hiyo ambayo inahitaji mikakati mizuri badala ya blabla.

“Huwezi kutenganisha maendeleo ya Shinyanga Mjini na Mbunge wa Jimbo.Tunayo mikakati mipango kabambe ‘Master Plan’ ya kuboresha mji wa Shinyanga ili uwe wa Kisasa. Kupitia Benki ya dunia tumepata kilomita 18 za barabara za lami mpya baada ya zile kilomita 13 za barabara za lami zilizojengwa.

Hizi kilomita 13 tu zimeufanya mji wa Shinyanga upendeze kiasi hiki ambapo kuna barabara za lami na taa zake je tukiongeza na kilomita 18 muonekano wa mji utakuwaje?,ndiyo maana nikisema Tunataka Shinyanga iwe mji wa Kisasa kuna baadhi ya watu hawanielewi kwa sababu hawajui mipango iliyopo”,alifafanua Masele.

Masele alisema mpango uliopo ni kuhakikisha kata zote za Jimbo la Shinyanga Mjini zinaunganishwa kwa barabara za lami na kuwaomba wananchi kutumia fursa ya mji wa Shinyanga kufanya shughuli za kujiinua kiuchumi.

Mbali na kutembelea kata ya Lubaga,Mhe. Masele ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP) akiwa ameambatana na Wajumbe wa kamati ya siasa Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Shinyanga mjini amekutana na Wajumbe wa kamati ya siasa Chama Cha Mapinduzi CCM wa ngazi ya matawi na kata ya Mjini na Kambarage.

No comments:

Post a comment