Wednesday, 18 December 2019

RC Adam Malima Afanya Ziara ya Kushtukiza Bukama


Mkuu wa mkoa wa Mara. Mh. Adam Malima amefanya ziara ya kushtukiza kiatika kijiji cha Bukama eneo linapojengwa hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Bunda vijijini ambapo amegundua mambo mengi ikiwemo kusuasua kwa ujenzi wa mradi huo huku chanzo kikidaiwa kuwa ni kutokuwajibika kwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Amos Kusaja.

Akiwa katika eneo hilo mafundi wamemwambia kuwa chanzo cha mradi huo kujengwa kwa kasi ndogo na kusuasua ni kutokana na ukosefu wa fedha na vifaa tatizo ambalo walidai kuwa linasababishwa na mkurugenzi wa halmashauri hiyo ambaye ameshindwa kutoa mahitaji kwa muda muafaka.

Wameadai kuwa licha ya kuwasilisha mahitaji kwa zaidi ya wiki tatu hakuna hatua iliyochukuliwa na mkurugenzi huyo huku wakidaia kuwa malipo kidogo ambayo pia hayatoki kwa wakati ni sababu nyingine inayokwamisha utekelezaji wa mradi huo.

" Mh. Mkuu wa mkoa toka ulipokuja hapa mwezi wa kumi ukatupatia pesa kwakweli ujenzi ulifanyika kwa kasi sana lakini baada ya pesa zile kukata tumerudia hali ile ile ya zamani mkurugenzi wala hana haraka licha ya kwamba siku ile ulimuagiza kuwa pesa na vifaa viletwe kwa wakati ili tukamilishe mradi huu" amesema fundi Chidaka Chidaka.

Kutokana na hali hiyo mkuu wa Mkoa amelazimika kuita kikao cha dharura cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa  ili kujadili halmashauri hiyo kutokana na kushindwa kukamilisha mradi huo licha ya maagizo ambayo amekuwa akiyatoa mara kwa mara.

Mh. Malima amesema kuwa Mh.  Rais Magufuli alitoa sh 1.5 bilioni kwaajili ya ujenzi wa hospitali hiyo kwa lengo la kusogeza karibu huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo ujenzi ambao uliotarajiwa kukamilika mapema mwezi Juni lakini hadi sasa haujakamilika bila sababu za msingi.

Mwezi Oktoba Mkuu wa Mkoa alifanya ziara katika eneo akiwa na pesa zake binafsi kwaajili ya kuwalipa mafundi hao ili ujenzi uweze kuendelea baada ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo kushindwa kutoa fedha bila sababu yoyote.

Kufuatua hali hiyo Mh. Malima aliagiza Takukuru kuchunguza matumizi ya fedha hizo kiasi cha sh 1.5 bilioni uchunguzi ambao bado unaendelea huku akimuagiza mkurugenzi huyo kufanya mambo kadhaa ikiwemo kupitia upya kwa pamoja na mafundi  mikataba ya ujenzi ambayo inaoenkana kuwakandamiza zaidi mafundi jambo ambalo amesema kuwa halikubaliki.

No comments:

Post a comment