NA MWAMVUA MWINYI, PWANI
INAELEZWA kuwa kati ya wilaya zinazoongoza kwa maambukizi makubwa ya VVU mkoani Pwani ni Kibaha Mjini ikifuatiwa na Mkuranga na Chalinze.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Pwani, katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi kimkoa ,huko Mwendapole ,Kibaha Mji,katibu tawala wa mkoa ,Theresia Mmbando aliwataka wakuu wa wilaya kushirikiana na wananchi kuweka mikakati na vipaombele ili kudhibiti maambukizi mapya ya VVU.

Aidha ,alisema mkoa huo unakabiliwa na baadhi ya changamoto zinazokwamisha juhudi za mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi ikiwemo kukosekana kwa mashine ya kupima wingi wa virusi vya Ukimwi ,biashara ya ngono,vigodoro na idadi ndogo ya vituo vya kutolea huduma ya kufubaisha VVU.
Theresia alibainisha ,pia ipo changamoto ya mila potofu katika jamii,ndoa za utotoni,maegesho ya malori,uzinzi,baadhi ya wana ndoa kutokuwa waaminifu na watu wanaojidunga madawa ya kulevya.

Hata hivyo alisema,hadi kufikia 2017, takwimu za kiwango cha maambukizi ni 5.5. Theresia alieleza licha ya hayo maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi miongoni mwa wanaume,wanawake na vijana ,vijana wenye umri kati ya miaka 15-49 ni mkubwa.

"Mwaka huu Januari -Oktoba maambukizi kwa wanaume yalikuwa 2,944 kati ya wanaume 133,832 waliopima maambukizi ya VVU sawa na asilimia 2.3."

"Kwa wanawake yalikuwa ni 5,145 kati ya wanawake 187,222 waliopima maambukizi ya VVU sawa na asilimia 2.7 na kwa upande wa vijana kuanzia miaka 15-24  maambukizi mapya ni 1,020 kati ya 95,559 waliopima sawa na asilimia 1.1"alieleza Theresia.

Nae mratibu wa masuala ya Ukimwi ,Kibaha Mjini Siwema Cheru alisema ,halmashauri hiyo inahamasisha jamii kuendelea kupata ushauri nasaha na kupima VVU na kwa wale wanaogundulika na maambukizi ya VVU kupata ushauri na kuanzishiwa dawa za kufubaza VVU .

Siwema alifafanua ,pia kuhamasisha WAVIU kujiunga kwenye vikundi ili kurahisisha utoaji huduma na hadi sasa kuna vikundi 17 vya watu wanaoishi na Ukimwi na VVU.

Kwa upande wake ,makamu mwenyekiti wa KONGA ,Kibaha Mjini,Antonia Mango,aliomba kupitia serikali za mitaa (TAMISEMI) itoe tamko kwenye halmashauri kutenga asilimia fedha za shughuli za UKIMWI kama ilivyofanya kutenga asilimia 10 kwa ajili ya vikundi vya wanawake,vijana na walemavu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: