Monday, 30 December 2019

KANISA LA ABC LA TABATA MANDELA LATOA VIFAA VYA SHULE KWA WANAFUNZI JIJINI DAR ES SALAAM


 Askofu Mkuu wa Makanisa ya Abundant Blessing Centre (ABC), Flaston Ndabila (wa pili kushoto), akikabidhi vifaa vya shule kwa mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Sekondari Zawadi, Irene Raina (wa tano kutoka kushoto), vilivyotolewa na kanisa hilo kwa wanafunzi 50 wasio jiweza na yatima jijini Dar es Salaam juzi. Wa kwanza kushoto ni Mfadhili wa msaada huo, Fanuel Leonard na wa tatu ni mke wa Askofu, Janeth Ndabila.
 Daftari zilizotolewa kwa wanafunzi hao.
 Askofu Mkuu wa Makanisa ya Abundant Blessing Centre (ABC), Flaston Ndabila, akizungumza na wanafunzi hao.
 Daftari na mafuta ya kujipaka yaliyotolewa kwa wanafunzi hao.
 Blandina Fanuel (kulia) akikabidhi msaada huo.
Advela  Fanuel (kulia) akikabidhi msaada huo.
 Wanafunzi wa kidato cha nne wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupokea vifaa hivyo. Kushoto ni Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mandela, Tablisa Bushir na kulia ni Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mandela, Leonard Chalema.
 Muumini wa kanisa hilo, Fanuel Leonard (kushoto), akimkabidhi mwanafunzi Mwanahamisi Bakari msaada huo. Kulia ni Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mandela, Tablisa Bushir.
 Mtoto Brown Fanuel (kushoto) akimkabidhi mwanafunzi Hassan Ally msaada huo.
 Wanafunzi wa darasa la sita wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupokea vifaa hivyo.
 Mke wa Fanuel, Oliva Fanuel akimkabidhi mwanafunzi Ziana Shabani msaada huo.
 Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mandela, Leonard Chalema, akikabidhi msaada huo kwa wanafunzi wa darasa la kwanza.
  Picha ya pamoja baada ya kupokea vifaa hivyo.
Ni furaha tupu baada ya kupokea msaada huo. 
Na Dotto Mwaibale
 KANISA la Abundant Blessing Centre (ABC) la Tabata Mandela  limetoa msaada wa vifaa vya shule kwa wanafunzi ambao ni ya yatima na wasiojiweza katika shule mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Wanafunzi waliopata msaada huo ni wa shule za msingi na sekondari kuanzia darasa la kwanza hadi la saba na kidato cha kwanza hadi cha nne ambapo kila mmoja wao alipatiwa madaftari tisa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana wakati wa kukabidhi msaada huo Askofu Mkuu wa Makanisa ya ABC, Flaston Ndabila alisema msaada huo umelenga kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Dkt. John Magufuli katika sekta ya elimu ya kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bure.
" Sisi kama kanisa tunampongeza Rais wetu kwa jitihada za kutoa elimu bure lakini tukaona kuna kundi la watoto wasiojiweza na yatima nasi tuwasapoti kwa kuwanunulia vifaa vya shuleni badala ya kuiachia serikali pekee" alisema Ndabila.
Alisema vifaa hivyo vimepatikana kwa kusaidiwa na familia ya muumini wa kanisa hilo Fanuel Leonard kwa ajili ya wanafunzi hao wakati wa kuanza  masomo mwezi Januari 2020. 
Alitaja vifaa hivyo kuwa ni madaftari, kalamu za kuandikia pamoja na mafuta ya kujipaka ambavyo vilitolewa kwa wanafunzi 50 katika shule hizo.
Alitaja wanafunzi waliopata msaada huo kuwa ni kutoka shule za sekondari za Pugu Kinyamwezi, Zawadi, Dar es Salaam, Zanaki, Tabata, Kigogo Mpeta, Kivule, Kambangwa, Oysterbay, Vingunguti na Mchikichini.
Kwa upande wa shule za msingi ni Tabata, Kawawa, Mtambani, Buguruni, Mkwawa, Kigogo CCM,  
Tabata Matumbi, Buguruni Moto, Kasulu, Buguruni Kisiwani, Mtambani, Amani, Kigogo na Uhuru Mchanganyiko.
Akipokea msaada huo Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mandela, Tablisa Bushir alimshukuru Askofu Ndabila kwa msaada huo na kuwa kanisa hilo linatakiwa kuigwa na watu wengine kwa kuwajali watoto wasiojiweza.
" Kanisa lenu ni la mfano tuna watoto wengi wenye mahitaji ya namna hii watu wengine wangekuwa wanajitoa kama mlivyofanya ninyi hakika tungewasaidia watoto wetu hasa wasio na wazazi na walezi" alisema Bushir.
Bushir aliwataka watoto hao kuzingatia masomo kwani elimu ndio urithi pekee wa maisha yao.
Muumini wa kanisa hilo, Fanuel Leonard alisema yeye na familia yake walitoa ahadi kwa Mungu kuwa mwaka huu watawasaidi watoto yatima na wasio jiweza kwa kuwanunulia mahitaji ya shule kama walivyofanya. 
Akitoa shukurani kwa niaba ya wenzake mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari ya Vingunguti, Samuel Boniface  alishukuru kanisa hilo kwa kuwapa msaada huo ambao umetolewa kwa wakati ukizingatia siku za kuanza msimu wa masomo 2020 zikiwa zimekaribia.

No comments:

Post a comment