NA HERI SHAABAN

Chuo Kikuu cha afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa ushirikiano na  Idara ya Afya Manispaa ya Ilala chini ya mradi wa "TCI"  tupange pamoja, (JHPIEGO)  wameanzisha klabu ya Afya kwa vijana.

Klabu hiyo imeanzishwa katika chuo cha MUHAS mwishoni mwa  wiki wakati wa mafunzo yalioandaliwa na Manispaa ya Ilala kutoa elimu kwa vijana  wa Chuo cha MUHAS  lililenga katika kutoa elimu, ushauri na burudani kwa vijana ili kuwajengea uwezo wa kujitambua na kufanya maamuzi sahihi kuhusu kulinda afya zao na hatimaye kufikia ndoto za  maisha yao. .
.

Akizungumza katika mafunzo hayo Mkufunzi  wa Chuo cha uuguzi Neema Nguno kwa niaba ya mgeni rasmi Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili , alisema  katika mafunzo hayo mada mbalimbali zilitolewa ikiwemo namna ya kukabiliana na  Rushwa katika vyuo vikuu, athari za ukatili wa kijinsia kwa vijana, udhibiti wa maambukizo ya Virusi vya UKIMWI na magonjwa ya ngono, Afya ya akili na athari za matumizi ya dawa za kulevya pamoja na huduma za rafiki za afya ya Uzazi kwa vijana na uzazi wa mpango.

 Neema alisema, wamehamasika zaidi kuunda klabu za afya chuoni hapo  baada ya baadhi ya wakufunzi wa shule za MUHAS kupata mwongozo na mafunzo ya afya ya uzazi kwa vijana kutoka Idara ya Afya Manispaa ya Ilala.

"Tumeona umuhimu wa vijana wetu kuwa na fursa ya kujadiliana na kubadilishana uzoefu,  elimu na changamoto kuhusiana na masuala afya ya uzazi kwa vijana kwa  kuanzisha klabu hii itasaidia kuendeleza juhudi za halmashauri ya Ilala katika kuimarisha huduma za afya ya uzazi kwa vijana" alisema Neema.

Alisema klabu hiyo  itasaidia kuwapa elimu na ushauri vijana kila wakati hapo chuoni ili kukabiliana na changamoto za kiafya zinazowakabili vijana zikiwemo mimba katika umri mdogo, mimba zisizotarajiwa, magonjwa ya ngono ikiwemo Maambukizo ya Virusi vya UKIMWI, utapiamlo kwa vijana, ukatili wa kijinsia na mbinu sahihi za namna ya kukabiliana na changamoto hizo.


Kwa upande wake Ofisa Mwandamizi wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Ilala, Damas Parsalaw alitoa elimu  kuhusiana na namna ya kupambana na  rushwa ikiwemo rushwa ya ngono kwa jamii.


 Alisema rushwa zipo za aina nyingi na mara nyingi ikihusisha makundi mbalimbali ya watu na taasisi katika jamii ambayo inaathiri kwa kiwango kikubwa maendeleo ya mtu binafsi, familia na taifa kwa ujumla.

 Alisema  vijana ni wajibu wo kupinga vitendo vyovyote vya rushwa katika sehemu zote za huduma hususani katika vyuo vyao.

Damas alisema kwa upande wa shule na vyuo angependekeza kuanzishwa kwa Klabu za kupambana na Rushwa kwa ajiji ya kuendelea kuwapa elimu zaidi na maelekezo ya namna ya kukabiliana na rushwa katika taasisi za elimu ya juu. Hii  itawasaidia zaidi katika kujiepusha na kushiriki kikamilifu katika Mikakati  ya kupambana rushwa katika chuo  na  katika ngazi ya jamii.

Naye Rais wa wanafunzi, Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Franco Joseph alisema elimu hiyo ni muhimu sana kwa vijana kwani vijana tunajikuta katika changamoto mbalimbali za kiafya kutokana na kukosa taarifa zilizosahihi hasa ukizingatia familia nyingi za kiafrika, wazazi hawapo wazi kuongelea masuala ya mabadiliko ya maumbile ya  vijana wao kutokana na mila na desturi za makabila mengi. Elimu na mkakati huu utakuwa endelevu baada ya kuanzisha forum ya kupata taarifa na  Elimu ya afya ya uzazi.

Franco alipongeza Halmashauri ya Ilala, Idara ya Afya kwa kuiweka MUHAS kuwa sehemu ya utekelezaji mkakati huo .

Alisema wanafunzi wengi hatuna ufahamu wa kutosha kuhusu na afya ya uzazi klabu iliyoanzishwa chuoni hapo itatusaidia katika kupeana elimu mara kwa mara .

"Klabu imeeanzishwa na wanafunzi wa vyuo vilivyopo  katika Taasisi ya Afya Shirikishi (IAHS) kwa kupitia Chama cha Wanafunzi (MUIAHSSO)" alisema Franco.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: