Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally amewataka wananchi kutumia haki ya kidemokrasia walionayo kujiandikisha na kuhuisha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

"Haki ya kidemokrasia inahusisha kuchagua na kuchaguliwa, na kigezo kimojawapo ni kuwa na kadi ya mpiga kura, hivyo kama sote tunahitaji demokrasia ya kweli, tujitokeze kujiandikisha na kwa wale waliohama maeneo yao ya awali nendeni mkahuishe taarifa zenu ili mtambulike eneo mnaloishi sasa,  kama mimi nilivyofanya leo, awali nilikuwa Dar es Salaam sasa nimehamia Dodoma"

Ameyasema hayo mapema leo alipokwenda kuhuisha taarifa zake katika daftari la kudumu la wapiga kura Kilimani jijini Dodoma ambapo kwa mkoa wa Dodoma uandikishaji utakuwa kati ya tarehe 06 -13 Desemba, 2019.

Awali, Katibu Mkuu amekutana na kufanya mazungumzo Makao Makuu Dodoma na ujumbe kutoka Chama Cha Kikomunisti Cha China (CPC) ukiongozwa na Prof. Wang Gang Naibu Mkurugenzi Mkuu Idara ya Utawala ya Chuo cha Taifa taaluma ya Utawala (National Academy of Governance),  mazungumzo hayo yamelenga maandalizi ya ufunguzi wa Chuo Cha Uongozi Cha Mwalim Nyerere na kuboresha zaidi mahusiano ya kihistoria kati CCM na CPC.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu amekutana na ujumbe kutoka Chama Cha kijamaa cha Viet nam (CPV) ukiongozwa na Mr. Pham Minh Chinh ambapo mazungumzo yamelenga kukuza mahusiano na kufungua fursa nyingine za ushirikiano.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Ndg. Humphrey Polepole na baadhi ya Maafisa wa Chama Cha Mapinduzi.

Imetolewa na;
Afisa Habari
Ofisi ya Katibu Mkuu
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM).
Share To:

msumbanews

Post A Comment: