Monday, 16 December 2019

ASILIMIA 80 YA WATANZANIA HULIMA KILIMO CHA HASARA


Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Waziri wa Kilimo Mhe.Japhet Hasunga amesema asilimia 80 ya Watanzania hulima kwa hasara hivyo kuna uhitaji mkubwa wa kuinua sekta ya kilimo ili wakulima walime kilimo chenye tija.
Mhe.Hasunga amesema hayo leo Disemba 16,2019 jijini Dodoma katika ufunguzi wa kikao cha Wataam mbalimbali wa kilimo hapa nchini wakiwemo Maafisa Ugani chenye lengo la kutathmini na namna ya kuboresha sekta hiyo.
“Wataalam wanasema heka moja ya mahindi  inatakiwa kuzalisha kuanzia gunia 25 na kuendelea lakini walio wengi wanazalisha gunia tano hadi kumi kwa heka na unakuta gharama anazotumia  katika utunzaji wa shamba ni zaidi ya  laki tano ndio maana Serikali imekuja na Mpango wa kuelelea sekta ya kilimo awamu ya pili ili kuhakikisha sekta ya kilimo inamnufaisha mkulima”.amesema.
Aidha Waziri Hasunga amesema serikali  haitapanga  bei ya Mazao huku akisema serikali bado ina uhitaji mkubwa wa Maafisa ugani ili kuendeleza sekta ya kilimo.
 Katika kutekeleza majukumu yao amewataka maofisa ugani kuhakikisha wanawatembelea wakulima na wafugaji kwa lengo la kuwapatia ushauri utakaowawezesha kulima na kufuga kwa njia ya kisasa.

"Inafika hatua unamkuta afisa Ugani anamuuliza mkulima kuwa hii ni mbegu gani,yaani baada ya ofisa ugani kumwelekeza mkulima, mkulima anamwelekeza Afisa ugani.

"Tunataka nyinyi maofisa ugani kuwa na takwimu za mashamba ambayo wanayakagua na kutoa maelekezo kwa wakulima kulima kwa kutumia mbegu bora.

"Kama maofisa Ugani mtakuwa karibu na wakulima na k├║wasaidia vyema ni wazi kuwa kilimo kitaongeza tija na kuwafanya wakulima kulima kilimo cha kisasa zaidi"alisema Hasunga.


Mwenyekiti wa chama cha wagani Tanzania ( Tanzania Socity of agriculture Educatiom and Extension TSAEE) profesa Catherine Msuya kutoka SUA amesema  chama hicho kilianzishwa mwaka 1984 kama jukwaa la wataalamu wanaojihusisha na kutoa elimu ya kilimo kwa wakulima wakiwemo maafisa ugani,watafiti,wakufunzi ,walimu wa kilimo ,viongozi wa wizara na taasisi  mbalimbali zisizo za Kiserikali huku akielezea wazo la kufufua chama hicho pamoja na lengo la mkutano huo.

Wakitoa salamu kwa niaba ya makatibu wakuu,Hilda Kinanga ambaye ni mkurugenzi wa Rasilimali watu wizara ya kilimo amesema wanaunga mkono kazi zinazofanywa na chama hicho huku Dkt Angelo Mwikawa  wa wizara ya mifugo na Uvuvi amesema akizungumza na kwa niaba ya Katibu Mkuu kilimo Olesant Ole Gabriel amesema nafasi ya wagani imekuwa na nafasi muhimu katika uendelezaji wa sekta ya mifugo na uvuvi.


Nao wabia wa Maendeleo ambao wamehudhuria katika mkutano huo Linda Temba wa Farm Radio International amekipongeza chama hicho kwani wao ni wadau wakubwa katika kilimo huku Michael Machera wa one Acre Fund akisema kuwa anaomba chama hicho kisife na wao waendelee kushiriki ili wawe wanaleta changamoto na kuzitatua kwa pamoja.

Serikali ya awamu ya tano chini ya Mh Rais Magufuli itaendelea kushughulikia changamoto  mbalimbali na itaendelea kutoa motisha na misukumo ya kutosha kwaajili ya uendelezaji wa sekta hizo muhimu.No comments:

Post a comment