Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amewaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii kusimamia uanzishwaji na uendeshwaji wa Kamati za ulinzi wa wanawake na watoto katika mikoa, Halmashauri, Kata, Vijiji na Mitaa yote nchini ili kuimarisha ulinzi wa wanawake na watoto ktk maeneo yote nchini.
Akizungumza katika uzinduzi wa Kampeni ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsi leo Jijini Dodoma, Waziri Ummy amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt John Pombe Magufuli imetekeleza kwa vitendo azma ya kukomesha vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto katika nchi yetu ambapo hatua mbalimbali zimechukuliwa ili kupambana na vitendo hivi ikiwemo kuendelea kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto 2017/2018- 2021/2022 . Mpango huu unalenga kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika Jamii yetu kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.
Waziri Ummy pia alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau imeongeza Vituo vya Mkono kwa Mkono vya Kutoa huduma kwa wahanga wa ukatili wa Kijinsia (One Stop Centres) kutoka vituo  4 mwaka 2015 hadi 13 mwaka 2019 ili kuwezesha utoaji wa huduma rafiki na kwa haraka  kwa wahanga wa ukatili.

Waziri Ummy ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na asasi za Kiraia katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa Kijinsia katika maeneo yote hapa nchini.

Aidha, Mhe Ummy ameagiza kuanzishwa kwa Madawati ya Jinsia Katika Taasisi za Elimu ya Juu ili kukomesha vitendo vya rushwa ya ngono na ukatili mwingine kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu. Aidha alisema kuwa kuanzishwa kwa madawati ya Jinsia na Watoto katika Vituo vya Polisi yapatayo 420 yamewezesha wahanga 58,059 kuripoti aina mbalimbali za matukio ya ukatili wa kijinsia kwa rika mbalimbali wakiwemo watu wazima na watoto katika matukio ya ubakaji, ulawiti, vipigo na ukeketaji.

Akizungumzia faida za madawati hayo Waziri amesema kuwa yameongeza mwamko wa wananchi katika kujiamini na kutoa taarifa za ukatili.

Kauli mbiu ya Kampeni ya siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia
Share To:

msumbanews

Post A Comment: