Wednesday, 6 November 2019

Wapinzani Watakiwa kuacha kutapatapa, kutoa kauli chafu kwa Serikali.

Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wilaya ya Ubungo Kissah Mbilla
Na Mwandishi Wetu.
VIONGOZI na wanachama wa vyama vya siasa vya upinzani wametakiwa kuacha kutapatapa na kutoa kauli chafu kwa viongozi wa serikali baada ya wagombea wao wanaowania nafasi za uongozi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuenguliwa katika hatua za awali za mchakato huo kwa kukosa sifa.
Kauli hiyo imetolewa leo na Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika wilaya ya Ubungo Kissah Mbilla wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Dar es Salaam.
Amesema kumekuwa na taarifa za upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii toka kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani kwamba wasimamizi wa uchaguzi huo wamewaengua kwa makusudi wagombea wao ili CCM wapite bila kupingwa jambo ambalo si kweli.
Kissah ameeleza kuwa wagombea wengi wa kambi ya upinzani walienguliwa katika mchakato huo kutokana na kutokuwa na sifa za kuwania nafasi hizo kwa mujibu wa Mwongozo na Kanuni za uchaguzi huo.
“Kilichowaengua si uonevu bali uelewa mdogo walio nao wa kutosoma Mwongozo na Kanuni za uchaguzi huo kama ilivyoelekezwa wakati wa kuchukua na kurudisha fomu za kuwania nafasi hizo.
“Niseme tu nasikitika sana kuona wagombea wengi wa vyama vya upinzani hawakuelewa chochote kuhusu kanuni licha ya kutoa elimu kwa viongozi hao na kuwapatia Kanuni na Mwongozo,” alifafanua Kissah.
Amesema kabla ya kuchukua na kurudisha fomu, Ofisi yake ilifanya semina kwa Makatibu na Wenyeviti wa Wilaya Kwa vyama 16 vya siasa katika ukumbi wa Manispaa ili kuwajengea uwezo na kwenda kutoa elimu kwa wagombea wao ili waweze kufuata taratibu za uchaguzi huo.
Amesema pamoja na jitihada hizo, wagombea wa upinzani hakuweza kuelimika huku wenzao wa CCM wakifanya vizuri.
Ameyataja baadhi ya makosa yaliyojitokeza katika ujazaji fomu kuwa ni pamoja na mgombea kujidhamini mwenyewe, majina kuwa tofauti kati yaliyowasilishwa na chama chake na kutojaza tamko mbele ya msimamizi wa uchaguzi kama ilivyoelekezwa katika fomu.
Mengine ni wagombea kurudisha fomu moja huku baadhi yao wakirudisha tatu na wengine wamerudisha nakala ya fomu badala ya ile halisi kama ilivyoelekezwa.
“Sasa makosa kama haya unaweza kusema kaonewa wakati tulitoa semina na maelezo ya kutosha kwa viongozi wao ngazi ya wilaya. Kwa nini wasiwalaumu viongozi wao?,” alihoji Kissah.
Amesema wagombea hao wanayohaki ya kupeleka mapingamizi yao ngazi husika ili yaweze kufanyiwa kazi na kwamba kulalamika tu mitaani bila kufuata taratibu za kisheria hakutowasaidia.
Amesema baadhi ya wagombea katika kata nne zilizopo wilaya hiyo tayari wamewasilisha pingamizi na yanafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria bila uonevu wa aina yoyote.
Amezitaja Kata zilizopokea mapingamizi ya wagombea hao kuwa ni Manzese, Ubungo, Sinza na Makuburi na kwamba mwisho wa kupokea pingamizi hizo ni leo.
Kissah amesema upotoshaji unofanywa sasa na baadhi ya viongozi unaweza kuleta chuki miongoni mwa Watanzania zitakazochochea vurugu zitakazopelekea uvunjifu wa Amani.

No comments:

Post a comment