Friday, 29 November 2019

WAHITIMU CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE WATAKIWA KUJITOFAUTISHA NA WAHITIMU WA VYUO VINGINE.


Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Stephen Wassira amesema Lengo la Chuo hicho ni kuendelea kuwa kitovu Cha Msingi wa maadili ili vijana wanaomaliza waweze kuwa viongozi bora katika Taifa.

Amesema hayo wakati wa mahafali ya 14 yaliyofanyika chuoni hapo ambapo wahitimu zaidi ya Elfu Tatu wametunukiwa Shahada zao.

Wassira amewataka wahitimu kuwa mfano wa kuigwa katika jamii kutokana na matendo yao na pia kuwa mabalozi wazuri ambao wanakiwakilisha vyema chuo katika Jamii zinaowazunguka.

“ Nendeni mkawe mabalozi wazuri katika Jamii na pia mkajitofautishe na wanafunzi waliomaliza katika vyuo vingine kutokana na maadili na nidhamu ambayo   mmejengewa  hapa chuoni” amesema Wassira ambaye ni Mwenyekiti wa bodi na mgeni rasmi wa mahafali hayo ya 14.

Amesema kuwa matendo ya vijana waliosoma Chuo Cha Mwalimu Nyerere yatatafsriwa katika Jamii  kuwa mmesoma Chuo chenye jina kubwa la Mwalimu Nyerere ambaye ni Baba wa Taifa la Tanzania.

Wassira amewataka vijana hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa lengo la kuondoka na umasinini na kuwa umasikini hauwezi kuondoka kama uchumi wetu haukui, huku akibainisha kuwa upo uchumi wa mtu mmoja mmoja na upo uchumi wa nchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila amesema dira ya Chuo hicho ni kuwa kitovu cha  utoaji wa maarifa bora kwa kutoa Elimu na mafunzo kuhusu ubunifu na uvumbuzi na kuendeleza amani na umoja wa kitaifa.

Prof. Mwakalila pia ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana chuoni hapo kuwa ni pamoja na
Kuboresha mazingira ya kufundishia, Kuongeza vitabu kwa kampasi zote na kuongeza udahili wa wanafunzi ambapo kwa sasa kwa kampasi zote mbili idadi ya wanafunzi imefikia 9,796.

Mkuu huyo wa Chuo ametaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa ukumbi wa mihadhara wenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 300 kwa mara moja, ufungaji wa vifaa vya kisasa vya kufundishia, idadi ya watumishi imeongezeka kutoka 230 kwa mwaka 2018 hadi kufikia 274, na idadi ya walimu imeongezeka kutoka 193 katika mwaka 2018 hadi 210 kwa mwaka 2019.

Imetolewa na:
Kitengo Cha Habari na Mawasiliano,
Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
29/11/2019

No comments:

Post a comment