Shule ya Msingi Mitundu B iliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi mkoani Singida ambayo viongozi mbalimbali na wadau wengine wamechangia ujenzi wake. 


Na Dotto Mwaibale, Singida. 

VIONGOZI wa Mkoa wa Singida wamechangia ujenzi wa Shule ya Msingi Mitundu B iliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi mkoani humo. 
Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,  Ally Minja alisema viongozi hao wamejitokeza na kutoa michango hiyo baada ya shule mama ya Mitundu kuzidiwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaoandikishwa shuleni hapo. 
Mwenyekiti huyo alisema Shule ya Msingi Mitundu B ilitokana na kugawanywa na shule mama ya Mitundu ambayo awali  ilikuwa na jumla ya wanafunzi 2566 wavulana wakiwa 1293 na wasichana 1273.
Minja alisema kutokana na msongamano huo wa wanafunzi uongozi wa shule kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Serikali ya Kata ya Mitundu pamoja na wadau mbalimbali wa Elimu kwa pamoja waliasisi ujenzi wa shule mpya ya Mitundu B kwa lengo la kupunguza msongamano huo. 
Alisema kutokana na juhudi hizo, uongozi wa mkoa uliamua kuunga mkono juhudi hizo, ambapo mkuu wa mkoa huo Dk .Rehema Nchimbi amechangia Sh. 750,000, Mwenyekiti wa  Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa, Mbunge wa Viti Maalumu Martha Mlata wamechangia sh. 2,250,000, Mkuu wa Wilaya ya Manyoni amechangia Sh. 500,000,  pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe ambaye ametoa sh.500,000.
Wengine ni Taasisi ya kifedha ya Benki ya NMB ambayo imechangia Sh. 5,000,000, Shirika la TEA (The Employers Association) limechangia Sh. 50,000,000, pamoja na wananchi waliojitokeza kushiriki katika zoezi hilo kwa namna mbalimbali. 
Kwa upande wake Mdau wa Maendeleo wa kata hiyo ya Mitundu Mhandisi wa Ujenzi, Felix Dagaki naye hakuwa nyuma katika kuhakikisha watoto wanajifunza kwenye mazingira tulivu yeye amechangia mifuko 20 ya saruji na sh.milioni moja  huku akiihimiza jamii kujitokeza kuchangia ujenzi wa shule hiyo. 
Share To:

msumbanews

Post A Comment: