Tuesday, 12 November 2019

Rais Magufuli nilinyweshwa sumuRAIS John Magufuli amefichua siri kuwa aliwahi kunyweshwa sumu wakati akiwa waziri wa ujenzi iliyomletea madhara na kwamba sababu ni kusifiwa kwa utendaji wake .

Amefichua siri hiyo leo Novemba 12, 2019 jijini Dar ea Salaam katika hafla ya uzinduzi wa kitabu cha maisha binafsi ya rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa.

‘‘Napenda kuweka wazi hili, nikiwa waziri wa ujenzi katika uongozi wa rais Mkapa niliwahi kunyweshwa sumu nikiwa mkoani Dodoma, hii ilitokana mzee Mkapa kunisifu kwa utendaji wangu mzuri wa kazi hadi kuniita mimi(Magufuli) ni mmoja wa askari wake wa mwamvuli wa ardhini,’’ amesema Magufuli na kuongeza.

‘‘Kutokana na tukio hili nilipana kujiuzulu nafasi hii lakini nilipokwenda kwa rais Mkapa kumueleza nia yangu hii, aliniangalia kwa jicho la huruma na kuniambia nenda kapige kazi na nilipewa ulinzi na kwa kweli ilinipa moyo na nikaendelea kuchapa kazi.’’

Amesema kutokana na kumbukumbu hiyo na yeye amejiwekea tahadhari ya kutowasifia sana mawaziri pamoja na watendaji ambao wanafanya vizuri ili kuwaepusha na changamoto za kuchukiwa.

Pamoja na mambo mengine akimzungumzia utendaji wa Mkapa, Rais Magufuli amesema alikuwa abagui viongozi aliowateua na kwamba ‘‘ Nilipokuwa naibu waziri wa ujenzi chini ya waziri Anna Abdallah, katibu mkuu mmoja alikuwa akidharua baadhi ya maelekezo yangu lakini Mkapa alimuagiza na kuyatekeleza kama nilivyomuelekeza.’’

Vilevile amewaomba viongozi na watanzania kwa ujumla kuandika vitabu ili kuweka kumbukukumbu sahihi ya maisha na historia binafsi na ya nchi.
Pia amewataka watanzania kuweka tabia ya kujisomea vitabu ili kuongeza maarifa.

Kitabu cha maisha binafsi ya Mkapa chenye kurasa 319 na sura 16 kimesimamiwa na taasisi ya Uongozi nchini na kimegharimu dola za kimarekani laki moja. Nakala moja ya kitabu hicho kitauzwa Tsh60,000

Miongoni mwa viongozi walihudhuria katika hafla hiyo ni rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Jakaya Kikwete, waziri mkuu mkuu, Kassim Majaliwa Spika wa Bunge Job Ndugai.

Wengine ni Maalim Seif Sharif Hamad, Jaji mstaafu Joseph Rarioba, Zitto Kabwe John Cheyo na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

No comments:

Post a Comment