Mvua iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha jana jioni Mkoani Songwe imesababisha uharibifu wa nyumba Zaidi ya 360 Katika Wilaya za Mbozi na Momba pamoja na kujeruhi watoto wawili.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen Nicodemus Mwangela mapema leo ametoa taarifa hiyo mara baada ya kukagua hali ya uharibifu wa makazi ya watu na taasisi za serikali ambapo ameziagiza halmashauri husika kurejesha miundombinu ya serikali iliyoharibika.

“Kuna wananchi wamepata madhara lakini wametibiwa na kurejea nyumbani, nawapongeza sana viongozi na majirani ambao waliwahi kutoa msaada kwa wahanga aidha ninaagiza halmashauri za Momba na Mbozi warekebishe haraka nyumba za walimu na madarasa ili huduma ziendelee.”, amesema Brig. Jen. Mwangela.

Aidha ametoa pole kwa wahanga  na amewapongeza majirani wa waliopata uharibifu wa nyumba kwa kuwahifadhi wenzao jana usiku huku akiwa hakikishia kuwa Kamati za Usalama za Wilaya na wataalamu wanafanya tathmini ya uharibifu na kupanga namna ya kutoa msaada.

Brig. Jen. Mwangela amewataka wananchi wote kuchukua tahadhari kwakuwa mvua za Mkoani Songwe ni nyingi hivyo waimarishe makazi yao pia watoe taarifa mapema endapo utatokea uharibifu wowote.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbozi Hanji Godigodi amesema wataalamu wa Halmashauri wanaendelea na tathmini ya hali ya uharibifu na kuwa nyumba za walimu na shule zitafanyiwa marekebisho haraka.

Afisa Mtendaji kata ya Msangano Halmashauri ya Wilaya ya Momba Focus Kadule amesema baada ya tathmini ya hali ya uharibifu katika kata yake ataitisha Mkutano wa hadhara ili wananchi waweze kujitolea kuwasaidia waliopata uharibifu kutokana na mvua hizo.

Fadeli Ng’aala mkazi wa Kijiji cha Hamwelo Halmashauri ya Mbozi amesema mvua iliyoambatana na upepo imeezua paa la nyumba yake huku yeye na watoto wakiwa ndani na kusababisha uharibifu wa vyakula na vifaa vingine kama vitanda, magodoro, televisheni, solar na masofa.

Naye Mwalimu Jacob Sambilila wa Shule ya Msingi Nkala Halmashauri ya Wilaya ya Momba amesema mvua zilianza saa tisa mchana na kusababisha mti kuangukia darasa hali iliyozua taharuki kwa wanafunzi lakini pia baada ya kurudi nyumbani kwake alikuta nyumba anayoishi imeezuliwa.

“Baada ya kutoka kazini nilikuta nyumba ya mwalimu mwenzangu imeezuliwa na nilipofika kwangu nimekuta nyumba imebomoka na kuezuliwa na kusababisha uharibifu hata kwenye chakula chote nilichotunza kimeharibika na vifaa vya ndani.”, amesema Mwalimu Sambilila.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: