Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Amiri Mruma Mruma (katikati) akipokea maelezo kutoka kwa Mkadiliaji Majenzi (QS) Yassin Khatib kutoka Mamlaka ya Majengo Tanzania(TBA) (wa pili kulia) akifuatiwa na Bw. Gaston Dindili , ambaye ni Fundi wa kampuni ya M/S Kiko Investment Ltd. Kushoto kwake ni Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Lushoto Mhe. Japhet Manyama akifuatiwa na Afisa Utumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto,Bw. Emmanuel Safari
Muonekano wa Jengo la Mahakama ya Mwanzo ya Mtae.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Amiri Mruma akisaini kitabu cha wageni katika Mahakama ya Mwanzo Mtae, kushoto ni Afisa Mtendaji wa Kata ya Mtae Bw. Miraji Bakari Msagati.
………………

Na Amina Ahamad- Tanga

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga Mhe. Amiri Mruma amesema Mahakama ya Mwanzo Mtae itafunguliwa haraka iwezekanvyo ili kuweza kutatua changamoto ya kutokuwepo kwa huduma hiyo katika eneo hilo.

Hayo yalisemwa na Mhe. Mruma wakati alipofanya ziara ya kikazi Novemba 25, mwaka huu kwenye mahakama hiyo ili kukagua ujenzi wa mahakama hiyo,utendaji kazi wa Mahakama ya Wilaya Lushoto, Mahakama ya Mwanzo Mnazi na Mlalo na shughuli za gereza la .la kilimo la Mng’aro.

Katika ziara hiyo Mhe. Jaji Mruma alitembelea na kufanya ukaguzi katika Mahakama ya Wilaya ya Lushoto ambapo alikagua usimikaji wa miundombinu ya huduma ya intaneti kupitia mkongo wa Taifa, usajili wa mashauri kwenye mfumo wakuratibu na kusajili mashauri kwa njia ya kielektroniki (JSDS 2) na ulipaji wa tozo na ada za kimahakama kupitia mfumo wa malipo wa Serikali (GePG).

Mhe. Jaji Mruma aliridhishwa na utendaji wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto chini ya Mhe. Japhet Manyama Hakimu Mkazi Mfawidhi ambapo alitoa pongezi.

Akiwa wilayani humo, Mhe. Jaji Mruma alipata fursa ya kukagua mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Mtae ulioanza tarehe 29 Desemba 2018.

Kwa mujibu wa tathmini ya mshauri elekezi, (QS) Yassin Khatibu alisema mradi huo umekamilika kwa asilimia tisini na tano (95) % ambapo tayari mfumo wa umeme umeshasimikwa na huduma ya maji safi imekamilika na maji yanapatikana kwa wingi.

Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtae, Fredson Masuke ambaye alimweleza Jaji Mruma kuwa kuwepo wa matukio mengi ya kihalifu yanayoripotiwa kituoni hapo, hali inayosababisha uhitaji mkubwa wa huduma za Mahakama.

Jaji Mruma aliahidi kufunguliwa mapema kwa Mahakama hiyo ili kesi zianze kusikilizwa na kutolewa maamuzi kwa misingi ya kisheria.

Hivyo itasaidia kupunguza matukio ya baadhi ya watu kujichukulia sheria mikononi, pale wasiporidhishwa na maamuzi ya baraza la kata na wengine kukata tamaa kupekeka kesi zao Mahakama ya Mwanzo Mnazi, Mlalo au Dochi kwa kukosa fedha za kusafiria zaidi ya kilometa 60.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: