Wednesday, 27 November 2019

Kampeni ya Kuhamasisha Vijana wa Kiafrika Kupanda Mlima Killimanjaro YaanzaNa Ferdinand Shayo,Killimanjaro.

Wadau kutoka Mashirika binafsi yanayojihusisha na masuala ya Vijana kutoka nchi za Zimbambwe,Uganda na Tanzania wameanza safari ya kupanda mlima Killimanjaro wakiwa na lengo la kuhamasisha vijana kutoka nchi 55 za Afrika kupanda mlima  huo  ifikapo May 2020  kama njia ya kuunganisha umoja wa bara la Afrika na malengo 2063  ya Afrika tunayoitaka.

Kiongozi wa Timu ya vijana hao Emanuel Motta kutoka kampuni ya Origin Trails ,alisema kuwa wamezindua kampeni ya kupanda mlima huo kwa kuanza kupanda mlima huo lengo ikiwa ni kufika kileleni na kutimiza adhma yao ya kuhakikisha kila kijana kutoka nchi za Afrika anapanda Mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika na wapili kwa dunia.

Aidha alisema kuwa vijana kutoka nchi za Afrika wanatarajia kupanda mlima huo wakifikisha ujumbe wa Afrika tunayoitaka na utekelezaji wake huku wengine wakiwa na mabango maalumu yaliyochorwa kwa usanifu unaoonyesha Afrika tunayoitaka.

Mkurugenzi wa Great Africa Art Banner  kutoka Zimbambwe, Munyaradzi Muzenda amesema kuwa kwa mara ya kwanza vijana kutoka nchi zote za Afrika watapanda mlima huo katika maadhimisho ya siku ya Umoja wa Afrika May 2020 kama ishara ya kuunganisha bara la Afrika na kudumisha umoja.

“Tunatarajia kuwa na idadi kubwa ya vijana watakaopanda Mlima mwakani Mlima Kilimanjaro utatumika kama nyezo ya kuliunganisha bara la Afrika kwa vijana kuungana kuwa na sauti moja,nguvu moja katika kusukuma gurudumu la maendeleo na kuhakikisha amani na mshikamano katika bara hili” Alisema Munya

Mwakilishi kutoka Shirika la Sister Sister Organization  lililopo nchini Uganda,Ayaa Musuya  alisema tayari wameanza kampeni ya kuhamasisha vijana kupanda mlima huo kupitia mitandao ya kijamii na kuwasajili kwa ajili ya zoezi hilo ambalo litaambatana na mashindano ya sanaa kwa vijana ya kuchora bango lenye picha ya Afrika tunayoitaka.

Anna alisema kuwa washindi watakaoibuka katika mashindano hayo wataungana na waliojisajili kupanda mlima huo na kupeleka bango litakaloshinda la Afrika tunayoitaka katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.

No comments:

Post a comment