Friday, 4 October 2019

Vituo 40 vya uokozi kujengwa ziwa Victoria


Na Ferdinand Shayo,Arusha.

Vituo 40 vya kuratibu shughuli za uokoaji  inapotokea dharura katika eneo la ziwa Victoria vinatarajiwa kujengwa lengo ni kunusuru maisha ya watumiaji wa ziwa hilo kwa uvuvi ama usafirishaji.


Halo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya fedha ya bunge la Afrika Mashariki ,Dokta Ngwaru Maghembe wakati akizungumza katika bunge la Afrika Mashariki lililofanyika mjini hapa.

Dokta Maghembe alisema kuwa,katika kukabiliana na changamoto hiyo nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki wamekuja na mradi mkubwa ambao utawezesha kuondokana na maafa hayo ambapo jumla ya vituo  vya kuratibu uokozi vipatavyo 40 vitajengwa katika eneo lote la ziwa hilo.

Alisema kuwa,mbali na ujenzi wa vituo hivyo pia kitajengwa  kituo kikuu mkoani Mwanza sambamba na kuwapatia simu  maalumu za mkononi wananchi wote wanaozunguka eneo hilo la ziwa ambao wamekuwa wakifanya shughuli za uvuvi  ,ambapo simu hizo zina uwezo  mkubwa wa  kutumika majini  pindi maafa yanapotokea na kuweza kutoa taarifa kwa haraka .

Dokta Maghembe alifafanua kuwa,mradi huo ulianza rasmi mwaka jana na unatarajiwa kumalizika  baada ya miaka mitatu na kukamilika kwa mradi huo mkubwa utaleta manufaa makubwa sana kwa wananchi hao sambamba na kuwawezesha  wananchi  kufanya uvuvi wao katika mazingira salama.

"pia napenda kuwashauri wananchi waishio katika ziwa hilo kujitahidi  kupanda miti ili kuweza kuzuia madhara yoyote yawezayo kutokea kwani wasipopanda miti hiyo wataendelea kusababisha madhara makubwa zaidi."alisema .

Aidha aliwaomba watanzania kulichukulia swala hilo kwa uzito mkubwa  kwani wao ndio watumiaji wakubwa  wa ziwa hilo katika kuwa mstari wa mbele kuchangia mradi huo kwani wenzetu wa Kenya na Uganda wanajitahidi sana kulichukulia uzito swala hilo.

No comments:

Post a Comment