Siku moja baada ya Rais John Magufuli kuongeza siku saba kwa washtakiwa wa makosa ya uhujumu uchumi, ambao hawajawasilisha maombi yao, Mwandishi wa Habari Erick Kabendera, anayekabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, amejitokeza kuomba radhi.

Ombi hilo lilitolewa jana na Wakili Jebra Kambole kwa niaba ya Kabendera, baada ya mwandishi huyo kupandishwa tena kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kufuatia makosa matatu yanayomkabili.

Mwandishi wa habari huyo alipandishwa kizimbani kwa madai ya kuongoza kundi la uhalifu kwa lengo la kupata faida au manufaa mengine, kutokulipa kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya zaidi ya Sh. milioni 173.2 na utakatishaji wa fedha kiasi cha zaidi ya Sh. milioni 173.24.

Wakili Jebra alidai Kabendera amemwomba radhi Rais Magufuli akieleza kwamba kama katika utekelezaji wa majukumu yake ya uanahabari kuna eneo alifanya makosa au aliteleza, amsamehe ili awe huru.

Aidha, Wakili Jebra alisema Kabendera yuko tayari kufanya jambo lolote, ili kulinda uhuru na usalama wake.

Kabendera, mwandishi wa habari za uchunguzi ndani na nje ya nchi, alichukuliwa na Jeshi la Polisi nyumbani kwake Mbweni, jijini Dar es Salaam Julai 26, mwaka huu, kabla ya kufikishwa mahakamani.

Katika kesi ya msingi,  mshtakiwa anadaiwa katika siku tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 2019 jijini Dar es Salaam, alitoa msaada katika genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

Katika shtaka la pili, inadaiwa siku na mahali hapo mshtakiwa bila kuwa na sababu za msingi kisheria alishindwa kulipa kodi ya Sh173.24 milioni ambayo ilitakiwa ilipwe kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika shtaka la utakatishaji fedha,  kati ya Januari 2015 na Julai 2019 ndani ya jiji na mkoa wa Dar es Salaam mshtakiwa alijipatia kiasi hicho cha Sh173.2 milioni wakati akizipokea alijua kuwa fedha hizo ni mazao ya makosa tangulizi ya kukwepa kodi na kujihusisha na genge la uhalifu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: