Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, CCM, Dkt Bashiru Ali, amewataka watumishi katika chama hicho kufanya kazi kwa moyo na kujituma ili chama hicho kiendelee kusimama na kuwa mfano kwa vyama vingine hapa nchini.

Pia amesema kuna mpango wa kuwakutanisha viongozi na wakuu wa idara zote ndani ya chama hicho wakae na kupewa mafunzo maalumu ya namna ya kazi na saikologia ya kila ya mtumishi ndani ya chama.

Dkt. Bashiru ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati wa kikao  baina ya katibu Mkuu CCM na watumishi wa Chama na Jumuiya zake, tukio lililoenda sambamba na kutolewa kwa vyeti kwa waliohudhuria mafunzo ya mpango mkakati wa miaka mitano, na kutolewa tuzo kwa mfanyakazi Bora wa Chama.

Amesisitiza watumishi ndani ya Chama kufanya kazi kwa moyo, kujituma na kwa kujitolea kwani kazi hizo zinahitaji kujitolea ili kufikia malengo wanayoyataka ndani ya chama hicho.

"Niwasisitize watumishi ndani ya chama kazi hii ni kubwa, inatakiwa mfanye kazi kwa moyo na kujituma na kujitolea kwa moyo, kwani kazi hizo zinahitaji moyo, kuna wengine mpaka wamepata vilema kwa ajili ya kazi za chama" amesema Dkt Bashiru.

Amewataka watumishi wote ndani ya chama kufanya kazi kwa kuhifadhi yale yote mazuri waliyoyakuta huku wakienda sambamba na kufanya Mabadiliko makubwa ndani ya chama ili kuendelea kujenga chama kiendelee kuwa na nguvu.

Amesema watumishi ndani ya chama wajenge utaratibu wa kujiendeleza katika mafunzo mbalimbali ambayo yatasaidia katika kufanyakazi kwa usitadi na kupeleka mbele maendeleo ya chama.

"Tuna mpango wa kuweka utaratibu kila mtumishi wa Chama lazima aoneshe kuwa kwa mwaka husika akipata mafunzo flani au amepata elimu kwa kujiendeleza kupanua upeo wake, Kama chama tunajenga vyuo mfano chuo cha Ihemi ili kujenga viongozi bora" amesema.

Pia amesisitiza watumishi ndani ya chama kuhakikisha wanatunza Siri za chama na kuhakikisha wanalinda nyaraka za serikali kama miiko ya kazi zao zinavyotaka, amewapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya ndani ya chama.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu bara, Lodrick Mpogolo, mbali na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na katibu ndani ya chama hicho, amesema pia amefurahishwa kuona vijana wengi katika watumishi kwamba huo ni mtaji mkubwa kwa kuwa na chama endelevu.

Amesema kwa sasa ndani ya chama kuna wataalamu wa vitengo mbalimbali hali inayosababisha chama kusimama na kujitegemea kwa kila kitu hali inayosababisha maendeleo ndani ya chama tofauti na hapo mwanzo.

" Sasa hivi ndani ya chama tuna wataalamu wa TEHAMA, na vitengo vingine vyote kwa Sasa vipo na hii inachangia maendeleo kwa sababu kw sasa tunategemea wataalamu wetu tofauti na hapo mwanzo" amesema Mpogolo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: