WMU – Ngorongoro, ARUSHA.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro uwaruhusu wananchi wa Kata ya Alaitole wajenge  shule ya wasichana ya bweni katika eneo la Esere lililo ndani ya Mamlaka hiyo ili waweze kupata elimu kufuatia wananchi hao kuzuiwa kwa muda mrefu kutekeleza mradi huo.

Aidha, ameutaka uongozi wa Mamlaka hiyo utoe kibali cha kuwawezesha wananchi kata hiyo kuanza ujenzi haraka iwezekanavyo ili fedha zilizotolewa na Serikali shilingi milioni 298 zianze kutumika.

Dkt. Kigwangalla ametoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza na kusikiliza kero za wananchi wa Kata Alaitole wilayani Ngorongoro kwenye mkutano wa hadhara uliowashirikisha viongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, viongozi serikali wa kata hiyo, viongozi wa mila wa kabila la Masai na madiwani na Mbunge wa jimbo la  Ngorongoro Mhe. William Ole Nasha.

Amesema Serikali inaunga mkono juhudi zote za wananchi za kujiletea maendeleo akifafanua kwamba hatua ya wananchi hao kuamua kujenga shule ya Sekondari ya Bweni ni jambo la linalopaswa kupongezwa na kila mpenda maendeleo.

“Mnacho kitaka kiko wazi, mnataka maendeleo ya watoto wenu, katika hili mmesema kila baba anatoa elfu hamsini na wanawake wanatoa elfu ishirini, hili ni jambo kubwa  achilia mbali nguvu kazi mnayojitolea na tayari serikali imeshaleta milioni 298, haiingii akilini eneo linalochangia kuleta na kuingiza mapato mengi Serikalini kiasi cha bilioni 126 likose shule” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.

Dkt. Kigwangalla ameeleza kuwa ujenzi shule hiyo utawaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono wananchi hao kwenye mipango yao ya utekelezaji miradi ya maendeleo.

Amesema jamii hiyo pamoja na mazingira wanayoishi kuwa ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wanahitaji elimu. Aidha, amesema pia ni muhimu katika sekta ya utalii kupitia utamaduni wao akiongeza kuwa kazi ya Wizara ni kuona mafanikio ya sekta ya utalii yanakuwa kwa kuongeza mapato na sio migogoro.

Dkt. Kigwangalla amesema Hifadhi ya Ngorongoro ni hifadhi mseto inayoruhusu binadamu na wanyama kuwepo katika eneo moja na kwamba hiyo ipo kwa mujibu wa sheria akiitaka Mamlaka hiyo kuyatazama vizuri majukumu yake ya kuendeleza Utalii, Kulinda rasilimali zililizopo kwa maana ya kuhifadhi na kuhudumia jamii iliyo ndani ya hifadhi hiyo.

Katika hatua nyingine ameutaka uongozi wa Mamlaka hiyo uendelee kufanya mazungumzo na wananchi hao badala ya kujielekeza katika matumizi ya nguvu ili kupata uelewa wa pamoja akitolea mfano wa eneo la Loliondo ambalo hivi sasa lina utulivu.

“ Viongozi wa Mamlaka mnalo jukumu la kuwasikiliza wananchi na kuamua kwa pamoja, eneo la Ngorongoro ni Urithi wa dunia na litaendelea kuwa hivyo kwa kuheshimu na maslahi ya Taifa na maslahi ya walio walio wengi” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.

Kuhusu mahusiano baina ya wananchi na wahifdhi Dkt. Kigwangalla amesema kuwa kupitia mkutano wake na wananchi amebaini kuwepo kwa tatizo la mawasiliano na mahusiano baina ya wananchi wa eneo hilo na  watumishi wa Serikali walio chini ya  Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro akibainisha kwamba tayari serikali imeliona jambo hilo na inaendelea kulifanyia kazi.

Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ngorongoro Mhe. William Ole Nasha akizungumza wakati wa mkutano huo amempongeza na kumshukuru Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha ulinzi wa rasilimali za Taifa katika maeneo mbalimbali nchini.

Amemwomba aeendelee kutembelea maeneo mengine ya jimbo hilo kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi wa kata za wilaya hiyo kwa lengo la kudumisha mahusiano mema.

Mhe. Ole Nasha ameeleza kuwa hatua ya Wizara kutafutia ufumbuzi mgogoro huo wa ujenzi wa shule ya wasichana ya bweni, vile vile uamuzi wa serikali kutoa eneo na fedha kiasi cha shilingi milioni 298 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo katika eneo lililokubaliwa ni ishara tosha kwamba Serikali inawalinda na kuwajali wananchi wake.

Amesema wananchi wa jimbo la Ngorongoro pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili wako ni wasikivu na wako tayari muda wote kushirikiana na Serikali ikiwemo ulinzi wa rasilimali zilizopo na kuendeleza uhifadhi katika hifadhi ya Ngorongoro.

Kwa upande wao wananchi wa Kata ya Alaitole wakizungumza kwa nyakati tofauti wamemshukuru Dkt. Kigwangalla kwa kuamua kuwafuata na kuzungumza nao katika makazi yao wakimpongeza kwa juhudi zake za kutatua changamoto mbalimbali kwa maslahi ya wananchi na uhifadhi.

Aidha, wamemwomba kuendelea kuisimamia sekta ya uhifadhi nchi wakitoa wito wa kudumisha mahusiano mema baina ya wananchi na wahifadhi.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: