Monday, 6 May 2019

Wanafunzi wa Kidato cha sita waonywa


Wanafunzi wa kidato cha sita na Ualimu wanaofanya mitihani leo wameonywa kutokujihusisha na wizi wa mitihani.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William ole Nasha leo Bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Nuru Awadh.

Mbunge huyo ametaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kutoa mafunzo ya Tehama kwa walimu na kutoa posho ya kufundishia ili waweze kuipenda kazi yao.

Akijibu swali hilo, Nasha amesema Tehama ni lazima kwa walimu wote na kwamba Serikali itaendelea kutoa elimu hiyo kwa sababu ni eneo muhimu la kujengewa uwezo.

Pia, amesema anawatakiwa heri wanafunzi wa kidato cha sita 91,442  na wale wa ualimu 12,540 wanaofanya mitihani yao leo nchini.

"Nawataka wafuate sheria na kanuni na kamwe wasije kujihusisha na wizi wa mitihani," amesema

Katika swali la msingi, Nuru alihoji Serikali ina mpango gani wa kurudisha utaratibu wa walimu kupigwa msasa.

Akijibu swali hilo, Nasha amesema Serikali imeendelea kutoa mafunzo endelevu kwa walimu kazini kulingana na upatikanaji fedha.

"Mafunzo haya yanalenga kuboresha utendaji na kutoa motisha kwa walimu ili kuondoa ubora wa elimu nchini," amesema.

No comments:

Post a comment