Wednesday, 1 May 2019

RAIS MAGUFULI AAHIDI NEEMA KWA WAFANYAKAZIAsema atawaongeza mshahara kabla hajatoka madarakani.

Rais Dkt. John Magufuli amewapongeza wafanyakazi nchini kwa juhudi wanazozifanya katika kazi na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi, kupanua uwekezaji katika miradi ya maendeleo na kutatua kero zinazo wahusu ili kulinda maslahi yao.

Dkt. Magufuli amesema hayo katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wafanyakazi (Mei Mosi) zilizofanyika katika uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya, baada ya kupokea maandamano  na kusikiliza risala ya wafanyakazi iliyosomwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Dkt. Yahaya Msigwa.

Amesema kwa kutambua kuwa wafanyakazi wana mchango mkubwa katika ujenzi wa uchumi wa Taifa, Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya kazi, hivyo ameridhia bodi ya mishahara kukutana ili isitumie vibaya fedha za umma, kupunguza viwango vya kodi ya mshahara (PAYE)  na kuwajali wafanyakazi wakiwemo wenye elimu ya Darasa la Saba.

“Nataka kuwahakikishia ndugu zangu wafanyakazi, Serikali ninayoiongoza inawapenda, hata hili la wafanyakazi wa Darasa la Saba nataka kuwajulisha kuwa kati ya wafanyakazi wote 525,506 walioajiriwa na Serikali wafanyakazi 98,615 wana elimu ya Darasa la Saba, Serikali haiwabagui wenye elimu ya Darasa la Saba” amesisitiza  Magufuli.

Kuhusu Maslahi na kupandishiwa mishara, Magufuli amewataka wafanyakazi kuwa na subira katika ombi lao la kuongezewa mishahara sababu serikali ina majukumu mazito ya kutekeleza miradi yenye gharama kubwa hivyo  ameahidi kuwaongezea mishahara hiyo kabla hajamaliza kipindi chake cha uongozi.

“Nawasihi ndugu wafanyakazi kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kuiletea maendeleo nchi yetu, Wazee wetu wa zamani walijitoa mhanga kuikomboa nchi yetu kisiasa, ni jukumu letu kizazi cha sasa kujitoa mhanga kuikomboa nchi yetu kiuchumi” amesisitiza Magufuli.

Sherehe za Mei Mosi mwaka huu zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mke wa Rais  Mama Janeth Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Job Ndugai, Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson, Mawaziri, Mabalozi, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Mikoa, Wabunge na viongozi wa Mkoa wa Mbeya wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Albert Chalamila.

Kesho, Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Mbeya ambapo atafungua Hospitali ua Uamsho wa Wakristo Tanzania (UWATA) na kuzungumza na wananchi wa Wilaya ya Mbarali katika uwanja wa Barafu Mjini Rujewa.

No comments:

Post a Comment