SERIKALI imesema maono na mtazamo yakinifu wa Rais Dkt. John
Magufuli katika usimamizi na ufuatiliaji wa sekta ya madini, umewezesha
ongezeko maradufu la makusanyo ya mapato ya sekta hiyo kutoka Tsh Bilioni 210
mwaka 2015/16 hadi kufikia Tsh Bilioni 302 kwa mwaka 2018/19 na kuifanya
Tanzania kuzidi kujijenga Kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari leo Alhamisi (Mei
30, 2019) Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na
Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, alisema Serikali ya Awamu ya Tano
inafanya kazi kisayansi na itahakikisha rasilimali za nchi zinaendelea kulindwa
ili ziweze kuleta manufaa kwa Watanzania wote.
Dkt. Abbasi alisema mara baada ya Serikali ya Awamu ya Tano
kuingia madarakani Novemba 2015, ilifanya mageuzi mbalmbali katika usimamizi na
ufuatiliaji wa rasilimali za madini, kwani huko nyuma Serikali ilikuwa
ikipoteza kiasi kikubwa cha fedha na kuamua kuchukua hatua stahiki ikiwemo
kufanya mabadiliko katika Sheria ya Madini ya mwaka 2010.
“Tulipofanya marekebisho katika sheria yetu ya madini mwaka
2017, matokeo tumeanza kuyaona kwani tumedhibiti mianya yote ya upotevu wa
mapato yetu na kuanza kusimamia kwa umakini mkubwa utoroshaji mkubwa wa madini
ambapo ilisababisha Serikali kupoteza kiasi kikubwa cha mapato” alisema Dkt.
Abbasi.
Akitolea mfano Dkt. Abbasi alisema kufuatia agizo la Rais Dkt.
John Magufuli la kuanzishwa kwa masoko ya madini ambayo ni utekelezaji wa
sheria ya madini ya mwaka 2017, hadi sasa kuna jumla ya masoko 24 ambayo
yamekuwa yakithibiti ubora, thamani na takwimu za madini nchini, ambapo soko la
kwanza lilianzishwa Mkoani Geita, mwezi Machi mwaka huu.
Aidha Dkt. Abbasi alisema Takwimu za jumla za uzalishaji wa
dhahabu katika kipindi cha miezi miwili , mkoani Geita kuanzia mwezi Machi hadi
Mei, mwaka huu zinaonyesha kuwa uzalishaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa na
kufikia kilo 312.65 za dhahabu ukilinganisha na uzalishaji wa
dhahabu kilo 259.12 zilizokuwa zikizalishwa kabla ya masoko hayo.
“Mwezi April, pekee uliweka rekodi ya Geita kwa kuzalisha kilo
200 ambazo hazijapata kufikiwa mkoani humo kwa wachimbaji wadogo na wa kati na
kwa Takwimu za Mei mwezi mwaka huu zinazidi kuthibitisha kuwa Watanzania
wanapaswa kuendelea kumuombea na kumuunga mkono Rais Magufuli” alisema Dkt
Abbasi.
Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi alisema eneo lingine la mageuzi
yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya madini ni pamoja na
maamuzi iliyochukua ya kujenga ukuta kuzunguka eneo la wachimbaji wa Madini ya
Tanzanite Mkoani Manyara ambao Serikali iliweka mifumo ya masoko na ukaguzi, na
hivyo kuchangia ongezeko la mapato ya wachimbaji wadogo na Serikali kwa ujumla.
Akifafanua zaidi Dkt. Abbasi alisema uzalishaji wa madini ya
Tanzanite kutoka kwa wachimbaji wadogo ulioripotiwa kwa mwaka 2016 ulikuwa kilo
164.6 na kilo 147 kwa mwaka 2017, ambapo Serikali iliweka kukusanya kiasi cha
Tsh Milioni 71 (2016) na Tsh Milioni 166 (2017), lakini uzalishaji huo
uliongezeka maradufu mara baada ya Serikali kujenga ukuta huo.
“Uzalishaji uliongeza sana mara baada ya ujenzi wa ukuta kwani
Kilo 781.2 zilizalishwa mwaka 2018 na kuiingizia Serikali mapato ya Tsh Bilioni
1.43 na uzalishaji kwa mwaka 2019 katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Mei
ulikuwa kilo 1086.05 zenye thamani ya Tsh Bilioni 1.422” alisema Dkt. Abbasi.
Post A Comment: