Sunday, 7 April 2019

WANYARANDWA WAANDAMANA KUADHIMISHA MAUAJI YA KIMBARI ARUSHA

Na Ferdinand Shayo,Arusha.
Mamia ya Wanyarandwa wamekusanyika na kuandamana katika viunga vya jiji la Arusha ikiwa ni ishara ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 25 tangu kutokea kwa mapigano na mauaji ya Kikabila Nchini na kusababisha mauaji ya maelfu ya Wanyarandwa.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini Arusha yanalenga kuhamasisha umoja na amani miongoni mwa wanyarandwa kuungana kama taifa bila kujali tofauti za kikabila .
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanyarandwa wanaoishi katika Mataifa mbalimbali duniani Murenzi Daniel amesema kuwa maadhimisho hayo yanalenga kuwakumbusha kudumisha amani na umoja kama nguzo muhimu ambayo kwasasa hawako tayari kuipoteza na wanawataka Wanyarandwa duniani kote kuungana
Tedy Shungushu ni Mnyarandwa anayeishi jijini Arusha amesema kuwa kumbukumbu hiyo ni ya muhimu kama taifa kujitafakari  na kuona namna ambavyo wanawakumbuka watu waliowapoteza katika mauaji hayo na kuwaenzi kila mwaka.
Kwa upande wao Watanzania walioshiriki katika maadhimisho hayo Maurin Njobi na Omega Urio wamesema kuwa yanawakumbusha kama Watanzania kudumisha amani na upendo na mshikamano kama taifa ili kuondoa uwezekano wa matukio kama hayo kutokea nchini
Zaidi ya watu Laki nane wanatajwa kupoteza maisha kwenye mauaji hayo ya Rwanda nchi ambayo kwa sasa inaongozwa na Rais wake Paul Kagame.

No comments:

Post a comment