Serikali imedhamiria kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi waishio mijini kufikia asilimia 95 na vijijini asilimia 85 ifikapo 2020.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mama Samia Hassan Suluhu wakati wa uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Aprili 2, 2019 zilizofanyika uwanja wa Kimondo – Forest Mlowo, Wilaya ya Mbozi, Mkoani Songwe.

Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2019 isemayo “Maji ni Haki ya kila Mtu, Tutunze Vyanzo Vyake na Tukumbuke Kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”

Makamu wa Rais amesema kuwa dhamira ya Serikali inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni  kuboresha huduma za jamii ikiwemo sekta ya elimu, afya, barabara,  umeme vijijini, usafiri wa anga, uvuvi, kilimo, viwanda na upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wote.

“Sera yetu ya Maji ya mwaka 2002 inasisitiza upatikanaji wa maji safi na salama ambayo ni muhimu kwa maisha ya kila mtu, shughuli za kiuchumi na ustawi wa mazingira,” alisema Makamu wa Rais.

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa maji safi, alieleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji nchini ikiwemo mabwawa ya kimkakati na kuboresha miundombinu ya uzalishaji na usambazaji maji safi.

Aidha, Makamu wa Rais alitoa wito kwa Wananchi kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji kwa kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kando ya vyanzo hivyo.

Kupitia hadhara ya Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Makamu wa Rais, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao ni muhimu katika kuleta maendeleo ya watu na huduma za kijamii.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: