Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Serikali imesema kuwa halmashauri ambayo haina uwezo wa kujiendesha kimapato ikiwa ni pamoja na uwezo wa kulipa posho za Madiwani haina sifa ya kuwa Halmashauri kwa mujibu wa Sheria na inapaswa kufutwa.
Hayo yamesemwa jana April 24,2019 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais na Serikali Mitaa ,TAMISEMI,Mwita Waitara wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbulu Vijijini Mhe,Flatei Grigory Massay aliyehoji kwa baadhi ya halmashauri kushindwa kulipa posho za Madiwani ,je,serikali ina mpango gani wa kubadilisha mfumo wa kuwalipa posho Madiwani kupitia hazina kama watumishi wengine huku pia akihoji mpango wa serikali kuanza kuwalipa posho Wenyeviti wa vijiji na mitaa kutokana na kazi kubwa wanayofanya.
Katika majibu yake Naibu Waziri wa TAMISEMI Mwita Waitara amesema halmashauri ambayo haina uwezo wa kujiendesha kimapato kwa mujibu wa Sheria inapaswa kufutwa na ametoa maelekezo kwa wakurugenzi kote nchini kuhakikisha wanalipa posho kwa madiwani huku akisema kuwa kila asilimia 20 ya Mapato ya ndani ya halmashauri inatakiwa irejeshwe vijijini ama mitaani hali itakayowezesha kulipwa wenyeviti wa mitaa na vijiji.
Hata hivyo Waitara amesema serikali inatambua kazi kubwa zinazofanywa na Madiwani ambapo mwaka 2012/2013 posho za madiwani zilipandishwa kutoka Tsh.laki moja na nusu[1,50,000] kwa mwezi hadi Tsh.laki mbili na nusu [2,50,000] kwa mwezi, kwa waraka wa mwaka 2012 sawa na ongezeko la asilimia 108.3%.
Mwaka 2014/2015 serikali ilipandisha posho za madiwani kupitia waraka wa mwaka 2014 kutoka Tsh.laki mbili na nusu[2,50,000] hadi Tsh. laki tatu na nusu [3,50,000] kwa mwezi sawa na ongezeko la asilimia arobaini[40%].
Vilevile Serikali inalipa posho ya madaraka kwa wenyeviti wa kamati Tsh.elfu themanini[80,000] kwa mwezi na posho ya kikao Tsh.elfu arobaini[40,000] kwa mujibu wa waraka wa mwaka 2007 na kigezo kinachotumika kupandisha posho za madiwani ni uwezo wa halmashauri kukusanya mapato.
Post A Comment: