Kamishna Mkuu wa kudhibiti fedha haramu hapa nchini Onesmo Makombe akizungumza na waandishi wa habari
 
Na Woinde Shizza, Globu ya jamii

NCHI za kusini na mashariki mwa Afrika zimetakiwa kuhakikisha kuwa zinabuni mbinu mbadala kuhakikisha kuwa zinakabiliana na tatizo la fedha haramu ambalo limekuwa likizidi kushika kasi katika nchi hizo.

Kamishna Mkuu wa kudhibiti fedha haramu hapa nchini Onesmo Makombe ameyasema hayo jijini Arusha jana alipokuwa akifungua mkutano wa maofisa wa kupambana na fedha haramu kutoka nchi za kusini na mashariki mwa Afrika.

Amesema kuwa suala la fedha haramu limekuwa ni changamoto kubwa katika nchi hizo na kueleza kuwa endapo juhudi makini hazitachukuliwa kukabiliana na tatizo hilo,itasababisha uchumi wan chi hizo kuzidi kushuka.

‘’Serikali za nchi wanachama zitatakiwa kukabiliana na biashara haramu za binadamu,madawa ya kulevya,rushwa na mengineyo yanayofanana nahayo kwani mambo hayo ndiyo yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa fedha haramu”alisema Makombe.

Ameshauri kila nchi mwanachama wa umoja wa kupambana na fedha haramu kwa nchi za kusini na mashariki mwa Afrika kuhakikisha kuwa itatunga sheria kali za kuhakikisha kuwa zinawabana wale wote wanaojihusisha na fedha haramu.

Awali,Mtendaji Mkuu wa kitengo cha kudhibiti fedha haramu hapa nchini,Eliamani Kisanga alisema kuwa lengo la mkutano huo ni kutengeneza sera na sheria za zitakazojikita zaidi kuhakikisha kuwa
nchi hizo zinakabiliana kikamilifu na tatizo hilo.

Amesema kuwa pia katika mkutano huo watajadili kwa kina ili kuhakikisha kuwa sheria zinazotumika kukabiliana na fedha haramu katika nchi wanachama zinafanana ikiwa ni pamoja na wahusika wanaopatika na makosa hayo kupewa adhabu zinazolingana katika nchi hizo.

Amesema kuwa mkutano huo utakaofanyika kwa juma moja unashirikisha nchi wanachama kumi na nane ambao unahudhuriwa na wajumbe zaidi ya mia mbili kutoka katika nchi hizo na kwamba mada mbalimbali zitawasilishwa na wajumbe watapata fursa ya kubadilishana uzoefu.

Alizitaja baadhi ya taasisi zinazoshiriki katika mkutano huo kuwa ni maofisa wa taasisi za kupambana na fedha haramu kutoka nchi wanachama,idara za mahakama,polisi,waendesha mashitaka,mamlaka za usimamizi wa bima,mabenki na malaka za kupambana na rushwa kutoka nchi
husika.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: