Wednesday, 17 April 2019

BUNGE LAKANUSHA UZUSHI KUHUSU CAG.

BUNGE la Tanzania limekanusha vikali taarifa zinazosambaa kupitia mitandao ya kijamii zinazo dai kuwa Spika wa Bunge Job Ndugai amemwandikia barua ya mashtaka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Assad, Bunge limesema taarifa hizo sio sahihi na znapaswa kupuuzwa.

Taarifa rasmi kutoka Bungeni zinaeleza kuwa uzushi huo umeanza kusamazwa mara baada ya Ndugai kukutana na kuzungumza na Waandishi wa habari kwenye Ofisi Ndogo ya Bunge Dar es Salaam mnamo tarehe 14 Aprili, 2019.

“Moja wapo ya taarifa hizo ni barua ya tarehe 14 Aprili, 2019 yenye mtindo wa kimashtaka yenye kichwa cha habari wito wa ama kujiuzulu au kujieleza kwa nini usiadhibiwe na mwajiri wako, inayodaiwa imeandikwa na Job  Ndugai, Spika wa Bunge kwenda kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Assad.”

“Tunapenda kuuarifu na kuutahadharisha Umma kuwa barua hiyo ni ya uzushi. Hivyo ipuuzwe. Ofisi ya Spika na Bunge kwa ujumla haihusiki kwa namna yoyote ile na barua hiyo iliyojaa uongo na uzushi.”

Aidha, imeutanabahisha umma kuhusu taarifa nyingine za upotoshaji ambazo zinaendelea kuwepo kwenye mitandao ya kijamii kuhusu suala hili zikimhusisha Spika na Bunge kwa jumla.

“Ufafanuzi kuhusu suala la CAG na Azimio la Bunge ulishatolewa na Spika Bungeni na katika kikao chake na Waandishi wa habari kilichofanyika Ofisi Ndogo ya Bunge, Dar es Salaam tarehe 14 Aprili, 2019.”

No comments:

Post a comment