Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali mara baada ya uzinduzi wa mradi wa kudhibiti Sumukuvu Tanzania (TANIPAC), ulifanyika katika ukumbi wa Kambarage uliopo katika jengo la Wizara ya Fedha na Mipango (HAZINA) Jijini Dodoma, Tarehe 12 machi, 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) aakisisitiza jambo wakati akizindua mradi wa kudhibiti Sumukuvu Tanzania (TANIPAC), ulifanyika katika ukumbi wa Kambarage uliopo katika jengo la Wizara ya Fedha na Mipango (HAZINA) Jijini Dodoma, Tarehe 12 machi, 2019.
Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa kudhibiti Sumukuvu Tanzania (TANIPAC), ulifanyika katika ukumbi wa Kambarage uliopo katika jengo la Wizara ya Fedha na Mipango (HAZINA) Jijini Dodoma, Tarehe 12 machi, 2019.
Katibu Mkuu wa Wiziri wa Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe akitoa maelezo ya awali kuhusu mradi wa kudhibiti Sumukuvu Tanzania (TANIPAC), ulifanyika katika ukumbi wa Kambarage uliopo katika jengo la Wizara ya Fedha na Mipango (HAZINA) Jijini Dodoma, Tarehe 12 machi, 2019.
Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikata utepe ishara ya uzinduzi wa mradi wa kudhibiti Sumukuvu Tanzania (TANIPAC), ulifanyika katika ukumbi wa Kambarage uliopo katika jengo la Wizara ya Fedha na Mipango (HAZINA) Jijini Dodoma, Tarehe 12 machi, 2019.

Na Mathias canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Watekelezaji wote wa Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu Tanzania- (Tanzania Initiatives for Preventing Aflatoxin Contamination – TANIPAC) wametakiwa kuhakikisha kuwa kunakuwa na matokeo chanya katika jamii katika utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha kuwa umasikini unapungua (Poverty reduction), na kujikita kutazama utekelezaji wa matokeo ya kama yatalingana na thamani ya fedha itakayotumika (Value for Money).

Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo Tarehe 12 machi, 2019 wakati akizindua mradi wa kudhibiti Sumukuvu Tanzania (TANIPAC), katika ukumbi wa Kambarage uliopo katika jengo la Wizara ya Fedha na Mipango (HAZINA) Jijini Dodoma.

Alisema kuwa, Mwezi Juni, 2018 Serikali ilizindua Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili au kwa kifupi ASDP II.  Programu ya ASDP II inalenga kuongeza tija katika uzalishaji, kukifanya kilimo kiwe cha biashara na kuongeza pato la mkulima ili kuboresha maisha, uhakika wa chakula pamoja na lishe.  Program hii inatekelezwa kikamilifu kupitia miradi mbalimbali ili kufikia malengo iliyojiwekea.

Mradi wa TANIPAC unatekelezwa chini ya vipengele (Component) Na. 2 na 3 ambavyo vinalenga kuongeza tija katika uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao.  Thamani ya mazao ni pamoja na chakula salama ambacho kinaenda kuuzwa kwa walaji ndani na nje ya nchi.  Na kwa kuwa ASDP II inalenga kukifanya Kilimo kuwa cha kibiashara, ni dhahiri mazao yanayotakiwa kuuzwa ni yale yaliyo salama. 

Alisema, utekelezaji wa mradi huo utasaidia katika kutimiza malengo ya ASDP II ambayo yana Kaulimbiu inayosema: Chakula ni Uhai. Tafsiri ya Kaulimbiu hii ni: - chakula salama ni msingi wa maisha, hivyo hapana budi kuimarisha mfumo wa uzalishaji wa chakula salama.

Waziri Hasunga alisema kuwa Suala la kuimarisha  biashara na masoko pamoja na uhakika wa chakula na lishe pia ni vipaumbele muhimu katika utekelezaji wa mpango wa uwekezaji na usalama wa chakula katika sekta ya Kilimo (Tanzania Agricultural and Food Security Investment Plan -TAFSIP) na Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo Bara la Afrika (Comprehensive African Agriculture Development Program – CAADP) kama ilivyoelekezwa kwenye Azimio la Malabo.

Kadhalika, suala la usalama wa chakula ni hitaji la lazima katika kufikia Malengo Endelevu ya Dunia (Sustainable Development Goals, SDGs), hususani Lengo Na.2.13.2 na 2.3 ambayo kwa ujumla yamelenga kukomesha njaa, kuhakikisha kuwa kuna usalama wa chakula na lishe, kilimo endelevu, kuimarisha afya na siha za watu nakupunguza upotevu wa chakula kwa kiwango cha asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

“Ili tuweze kuelewana vizuri nataka tutofautishe dhana ya usalama wa chakula (food security) na chakula salama (food safety).  Mradi tunaozindua leo ni wa kuhakikisha chakula tunachozalisha, tunachouza na tunachokula ni salama kwa maana ya kutokuwa na sumu inayoweza kuathiri afya za watumiaji.  Usalama wa chakula ni hali ya kuwa na uhakika wa chakula cha kutosha na chenye viini lishe vya kutosha katika ngazi ya kaya na Taifa” Alikaririwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa

“Ni muhimu tukafahamu kuwa, suala la chakula salama (food safety) ni tatizo Duniani kote na huathiri mataifa yote, hasa yale yanayoendelea kama Tanzania na nchi nyingine za dunia ya tatu. Hii inatokana na kutokuwa na mifumo imara ya usimamizi katika nyanja za uzalishaji wa chakula, uhifadhi na ugavi”

Mhe Hasunga alieleza kuwa Changamoto hiyo ya chakula salama inachangia kwa kiasi kikubwa kudhoofisha afya za Walaji, wakati mwingine vifo na athari nyingine nyingi zikiwemo za kiuchumi.

Tatizo la sumukuvu si geni katika Ukanda wa Afrika Mashariki Kwa mfano, tatizo hilo limekuwa likijitokeza mara kadhaa katika nchi ya Kenya ambapo mwaka 2004 watu zaidi ya 300 walipata ugonjwa wa Aflatoxicosis utokanao na sumukuvu na kusababisha vifo vya Watu 125 baada ya kula chakula kilichokuwa na kiwango kikubwa cha sumukuvu.

Tatizo kama hilo liliwahi kutokea nchini mwaka 2016 ambapo zaidi ya watu 60 katika Halmashauri za Bahi, Chemba, Kiteto na Kondoa waliugua baada ya kula chakula chenye kiwango kikubwa cha sumukuvu na watu 19 kufariki kwa tatizo hilo. 

Mradi wa TANIPAC ambao umezinduliwa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga unalengo la kupunguza sumukuvu (aflatoxin) katika mazao ya mahindi na karanga. 

Aidha, Taarifa zinaonesha kuwa tatizo la Sumukuvu ni kubwa kwani inakadiriwa kuwa asilimia 25 ya mazao yote yanayozalishwa duniani yanaathiriwa na Sumukuvu. 

Tafiti za kiafya zinabainisha kwamba, sumukuvu huchangia zaidi ya aina 25 za saratani na kipekee inachangia asilimia 30 ya saratani ya ini.  Pamoja na kuchangia saratani, kuna ushahidi wa kisayansi unaoonesha kwamba sumu hiyo huchangia udumavu kwa watoto ambapo  yanaathiri ukuaji wa mtoto kimaumbile pamoja na kuchangia kudumaa kwa akili.  Vilevile, tatizo la sumukuvu huathiri biashara ya mazao ya chakula katika soko la Kimataifa ambapo kwa Bara la Afrika linapoteza zaidi ya Dola za Marekani Milioni 670 ambayo ni sawa na asilimia 40 ya mauzo yote ya nje yanayokataliwa kila mwaka.

Share To:

Post A Comment: