Na. Elinipa Lupembe.
Wanawake halmashauri ya Arusha, wametakiwa kubadili fikra na kujikwamua kimtazamo, kiuchumi, kisiasa, kijamii pamoja na kuhakikisha wanazingatia upatikanaji wa lishe bora kwa familia zao na jamii kwa ujumla ili kuwa na taifa lanye afya bora kwa maendeleo endelevu,  katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, yaliofanywa na halmashauri ya Arusha, kwenye viwanja vya shule ya sekondari Enaboishu kata ya Moivo,
Akizungumza wakati wa sherehe hizo,  mgeni rasmi ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii, mkoa wa Arusha, Irene Mateu amewataka wanawake hao, kubadili fikra na mitazamo yao, na kutumia fursa zinazotolewa na serikali na wadau mbalimbali ili kujikwamua wenyewe katika sekta zote na kutekeleza majukumu yao kama wanawake.
Amesema kuwa, wanawake wanapaswa kutambua, wao ndio msingi wa mabadiliko katika jamii na endapo watabadili fikra na mitazamo yao kuwa chanya, ni dhahiri kutakuwa na taifa bora lisilo na ukatili na udhalilishaji wa wanawake,  na kutokomeza tatizo la  ndoa na mimba za utotoni, pamoja ukeketaji kwa wanawake
Irene amesisitiza kuwa, wanawake wanapaswa kusimama imara kupinga  na kuwafichua watu wanaofanya ukatili wa kijinsia na wale waliofanyiwa ukatili, ili kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto na sio kuungana nao kuwaficha wahalifu hao.
" Inatupasa kutambua, wanawake ndio msingi wa mabadiliko kwenye jamii, kama wanawake tutabadili fikra zetu na kutekeleza majukumu yetu kwa usahihi, kuanzia ndani ya  familia zetu, jamii zatu zitabadika pia, hakutakuwa na ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto, watoto wetu hawatakeketwa wala ndoa na mimba za utotoni hazitakuwepo" amesema mgeni rasmi huyo.
Aidha mgeni rasmi huyo, amewataka wanawake hao kutumia majukwaa ya wanawake katika maeneo yao, kwa kukutana na kubadilisha uzoefu katika nyanja mbalimbali, kuambukizana ujuzi na maarifa kwenye fani mbalimbali, kwa lengo la kubadili fikra hasa katika kuwakwamua kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa maendeleo endelevu.
Naye Diwani wa Viti Maalum, Mhe. Yasimin Bachu amesema kuwa, imefika wakati sasa wanawake kuchukua hatua la haraka kuhakikisha familia na jamii zao, zinapata lishe bora pamoja na ufanyaji wa mazoezi ya mara kwa mara ili kuimarisha afya na kuepuka magonjwa yasiyoambukiza, magonjwa ambayo yanakwamisha na kurudisha nyuma gurudumu la maendeleo katika taifa letu.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Afisa Maendeleo ya Jamii na Jinsia, Halmashauri ya Arusha, Getrude Darema, amesema kuwa, halmashauri hiyo imefanya maadhimisho hayo, huku ikiwa na mafanikio makubwa katika kuwawezesha wanawake kiuchumi,  jumla ya wanawake wajasiriamali 395 kwenye vikundi 45, kwa kuwapatia mikopo ya bila riba, yenye thamani ya shilingi milioni 243, fedha zinazotokana na asilimia 4 za mapato ya ndani kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019.
Hata hivyo Getrude,  amesema kuw, halmashauri inatarajia kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 80 kwa vikundi nane zaidi hadi kufikia mwishoni mwa wiki hii na kuwahimiza wanawake kutumia vyema fursa hiyo kwa kuanzisha miradi ya kibiashara itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi na si vinginevyo.
Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu ya "Badili Fikra Kufikia Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu"   na maonesho mbalimbali ya biashara kwa wajasiriamali wanawake, upimaji wa afya kwa magonjwa yanayoambukizwa na yasiyoambukizwa bure, burudani mbalimbali,  mashindano ya mchezo ya kuvuta kamba na kufukuza kuku, pamoja na mafundisho ya uandaaji wa chakula lishe.
MATUKIO KATIKA PICHA.


Share To:

msumbanews

Post A Comment: