Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akikabidhi mkopo kwa mmoja wa wanakikundi cha Mshikamano kutoka kijiji cha Chala katika hafla fupi ya utoaji mikopo katika Halmshauri ya Wilaya ya Nkasi ambapo vikundi 15 vilipatiwa mikopo ya jumla ya Shilingi milioni 53.


Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda akitoa nasaha zake kwa wanavikundi wajasiliamali waliopewa mikopo (hawapo pichani) wakati wa hafla fupi ya kutoa mikopo hiyo

 Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa nasaha zake kwa wanavikundi wajasiliamali waliopewa mikopo (hawapo pichani) wakati wa hafla fupi ya kutoa mikopo hiyo.

Wawakilishi wa vikundi vya Wanawake, vijana na walemavu wakipokea hundi ya mfano yenye thamani ya shilingi milioni 53 kutoka kwa mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo (kaunda nyeusi) katika hafla fupi ya kukabidhi mikopo hiyo kwa vijana.

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wajasiliamali wa Wilaya ya Nkasi kuhakikisha fedha ya mkopo waliyopewa na halmashauri hawazitumii katika matumizi binafsi bali wazielekeze katika biashara ili ziweze kuwapatia faida na kuwainua kiuchumi na hatimae kupata fedha za kujikimu kimaisha.
“Kwenye vikundi vyenu mna malengo mahususi na ili haya malengo mahususi yaweze kutimia kwenye biashara hakuna kingine zaidi ya kuwa bahili lazima muwe mabahili, lazima muwe watu ambao hamkubali kutoa fedha hovyo hovyo, uskibali kutoa fedha ambayo haina mpango, leo unaambiwa kuna msiba pale wewe unachukua fedha ya mkopo unapeleka, huu sio ubahili, weka fedha yako vizuri, kama kuna shida tafuta hela nyingine,na ukichukua fedha inayotokana na hapo labda ni faida,” Alisema.
Ameyasema hayo alipokuwa akikabidhi mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 53 ikiwa ni asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani ya halmashauri kwa vikundi 15 vya halmashauri ya wilaya ya Nkasi ikiwa ni utekelezaji wa kisheria chini ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) lililoanzishwa Mwaka 2005 chini ya sheria na 16 ya mwaka 2004 yenye adhima ya kuwainua wananchi kiuchumi ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Katika kulisisitiza hilo Mbunge wa jimbo la Nkasi Kaskazini Mh. Ally Kessy alisema kuwa pesa hizo ni kodi za wananchi ambazo halmashauri inapita kuzikusanya nahatimae asilimia 10 ya mapato hayo kuyagawa kama mikopo kwa wajasiliamali wanawake, vijana na walemavu na kusisitiza kuwa fedha hiyo irudishwa kadiri inavyotakiwa.
“Fedha hii ni mkopo na sio sadaka, isiwe kukopa harusi na kulipa matanga, kulipa ni wajibu, hizi pesa sio sadaka ni kodi ya wananchi na kodi ya wanachi haiendi bure, mnakopeshwa mkafanye maendeleo sio muanze kununua magauni au kwenda harusini hakuna ni kufanyia mtradi, kama unaona kikundi chako hakina uwezo na kulipa msichukue ili wapewe wengine,” Alisisitiza.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Emanuel Sekwao wakati akiseoma taarifa alisema kuwa Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Jumla ya vikundi 15 viliomba mikopo ya Tshs. 68,292,000.00. lakini baada ya Kamati ya Mikopo kukaa na kupitia maombi ya mikopo jumla ya kiasi cha Tshs 53,000,000 kiliidhishwa.
 “Vikundi vitakavyokopeshwa ni 15 ambapo Vikundi vya Vijana vitatu Jumla ya fedha Tshs 12,687,000 Kikundi cha Walemavu kimoja, Jumla ya fedha Tshs 2,000,000 na Vikundi vya Wanawake kumi na moja, jumla ya fedha Tshs 38,313,000. Vikundi hivyo vimetoka katika kata za Mashete, Kipundu, Majengo, Sintali, Namanyere, Chala, Kipande, Kabwe, Kate, Kirando na Kala.”
Nae mkuu wa wilaya hiyo Mh. Said Mtanda alimuhakikishia mkuu wa mkoa kuwa watajitahidi kuhakikisha wanakusanya mapato ya halmashauri kwa asilimia 100 na kutoa mikopo hiyo kwa vijana na kuwapa fursa ya kujiajiri lakini pia kuongeza viwanda vidogovidogo kutokana na shughuli mbalimbali za uzalishaji wanazojihusisha nazo wajasiliamali hao.
Katika kutoa shukrani mmoja wa vijana wa kikundi cha Panda Miti Rukwa (PAMIRU) Uswege Mwasomola alisema kuwa lengo lao ni kuwa na shamba la miti la kikundi ili kusaidia kutunza mazingira na kuongeza kuwa kutokana na mkopo huo walioupata wataweza kutatua changamoto walizokuwa nazo kwa asilimia 100.
“Mkuu wa Mkoa pamoja na viongozi wote nadhani mwaka ujao hatutakuja kukimbizana kufuatilia mikopo zaidi tutakwenda kifua mbele kwa kuhakikisha tunairudisha kwa muda muafaka ili tutoe fursa kwa vijana wengine,” alisema.
Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi katika mwaka wa fedha 2018/2019 inatarajia kukusanya jumla ya Tshs 2,304,000,000/= kupitia vyanzo vyake vya ndani. Katika kipindi cha kuanzia Julai 2018 hadi Februari 2019 jumla ya Tshs 1, 511,915,838.67 ilikusanywa ambapo sawa na asilimia 65.62 ya bajeti ya mwaka wa fecha 2018/2019.
Share To:

Post A Comment: