Rais Mstaafu wa awamu Tatu  Benjamin William Mkapa amekipongeza Chuo Kikuu kishiriki cha Jordan JUCo kwa kutimiza jubilee ya miaka 25 ya utoaji huduma ya Elimu ya Juu nchini  na kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa Chuo hicho na vyuo vingine binafsi katika kuwezesha upatikanaji wa elimu nchini hususan elimu ya juu .

Mh. Mkapa amesema hayo katika kilele cha sherehe za Jubilee  zilizofanyika katika Chuo hicho jijini Morogoro na kuhudhuriwa wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi. Aidha amesema pamoja na kazi nzuri wanayofanya vyuo Binafsi ada zinazotozwa katika vyuo hivyo bado ziko juu, hivyo amevitaka kuhahakisha wanajiendehsa kwa gharama nafuu bila kuathiri ubora na kuhahakikisha wanatoza ada kwa viwango ambavyo Watanzania walio wengi watamudu na kuweza kupata elimu hiyo kwa maendelo yao na taifa kwa ujumla.

“ Nisema kuwa Elimu pekee ndiyo inachangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na baade Taifa kwa ujumla, hivyo ni vyema garama za ada ziwe ni zile ambazo wananchi wa kawaida watamudu, ikumbukwe kuwa wananchi waliowengi wanategemea mikopo inayotolewa na Serikali, sasa Vyuo binafsi ni vyema ikaliangalia hili,”alisema Mzee Mkapa.

Awali akizungumza katika Jubilee hiyo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya utoaji elimu ya juu ili kuongeza bora na kuwa haitavifumbia macho vyuo ambavyo havitatii na kuzingatia vigezo,Sheria, taratibu na kanuni za uendeshaji wa vyuo hapa nchini.

“ Nitoe wito kwa vyuo vyote nchini kuhakikisha vinakidhi vigezo vya uendeshaji wa vyuo, tofauti na hapo serikali haitasita kuchukua hatua stahiki kwa vyuo vitakavyokwenda kinyume. Lengo la serikali ni kuhakikisha Elimu bora inatolewa nchini ili kuzalisha wataalamu wenye uwezo na maarifa kwa ukuaji wa uchumi,”alisema Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako amesema hadi sasa Tanzania kuna vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki 49 ambapo kati ya hivyo  34 ni vyuo binafsi ambayo ni sawa na asilimia 69.4 . Hivyo Serikali inatambua mchango wa mkubwa wa Vyuo binafsi na amekipongeza Chuo Cha Jordan kwa kutumiza miaka 25.

Aidha Waziri Ndalichako alisisitiza pia kuwa serikali inaendelea kuimarisha Bodi ya mikopo ili kutoa mikopo zaidi kwa wanafunzi ambapo alisema kumekuwa na ongezeko la idadi ya Wanafunzi wanaopata mikopo  hiyo ambapo kutoka mwaka 2004/05. hadi  mwaka 2018/19 wanufaika wa mikopo kwa ujumla ni 480,405.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Steven Kabwe  amesema Chuo Cha Jordan kutimiza miaka 25 ni hatua kubwa na kuwa Chuo hicho ni miongoni mwa vyuo vya mfano katika mkoa huo kwa sababu mkoa haujawahi kupokea taarifa za wananfunzi wa Chuo hicho kujihusisha na Makundi wala vitendo viovu. Aidha ameahidi kushirikiana na chuo hicho kwa kutumia watalaam wanaoandaliwa hapo kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa.

Imetolewa na:

KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI,
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
14/3/2019
Share To:

msumbanews

Post A Comment: