Mbunge Jimbo la Nyamagana Mhe. Stanslaus Mabula ameungana na wanawake takribani 1,000 wilayani Nyamagana kuadhimisha siku ya wanawake duniani kupitia maonesho ya bidhaa pamoja na Kongamano maalum lililowakutanisha wadau wa maendeleo ya wanawake, taasis za fedha, taasis za wanawake, vikundi vya wajasirimali, baraza la wanawake Wilaya pamoja na Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi wilaya na mkoa wa Mwanza.

Akifungua maadhimisho haya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt. Philip Nyimbi amewaasa wanawake kutochagua kazi ili kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali, pamoja na kulea watoto katika mazingira ya kupenda masomo yenye michepuo mbali mbali hususani sayansi itakayowezesha kufanya kazi yeyote siku za usoni. Kadhalika Dkt. Nyimbi ameelekeza afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya Jiji la Mwanza kutoa elimu ya ujasirimali na mikopo kwa makundi yote ya wanawake ambayo hayajafikiwa na mikopo ili waweze kunufaika na tengo la asilimi 10 ya mapato ya halmashauri kupitia mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Vijana na Walemavu kwani kupitia maonesho imedhililisha mahitaji ya mitaji ni mengi.

Akisoma risala kwa mgeni rasmi kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji la Mwanza, Afisa maendeleo ya Jamii amesema maadhimisho haya yanafanyika duniani nzima toka Mwaka 1945 Umoja wa Mataifa ilipitisha siku ya tarehe 08.03 kuwa siku ya wanawake Duniani, ambapo kila mwaka imekuwa ikitoa kauli mbiu na kutafasiliwa nchi husika kwa kuakisi mahitaji yao. Na kwa mwaka 2019 kauli mbiu ni *Badili fikira kufikia usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu* Ambapo kilele cha maadhimisho haya itakuwa siku ya tarehe 8 Machi, na kimkoa itafanyika Kata ya Kisesa wilayani Magu.

Akiongea kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania mkoani Mwanza Bi. Agnes ameipongeza serikali kupitia halmashauri ya Jiji la Mwanza kuwa ya mfano kwa kujiwekea utaratibu mzuri unaowezesha wanawake kukuza mitaji yao kupitia mfuko wa maendele ya Wanawake, Vijana na Walemavu. Ametumia fursa hiyo kuziomba halmashauri nyingine kuiga mfano huu unaowawezesha wanawake wapate mikopo isiyokuwa na riba kukuza mitaji kwa wakati.

Akitoa salamu za Mhe. Stanslaus Mabula Mbunge Jimbo la Nyamagana, Bi. Florah Magabe, amesema Mhe. Mabula anawapongeza wanawake wa Nyamagana ambao 78% ya waliokopa fedha za halmashauri wamerejesha kwa wakati na wamedhihilisha wanakopesheka na wapo tayari kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo, ufugaji, uvuvi pamoja na uongezaji wa thamani kupitia malighafi ya ndani ambayo ndio falsafa halisi ya taifa tunapoelekea *Uchumi wa Viwanda*.

Maadhimisho haya yamefanyika chini ya Mwenyekiti kamati ya maandalizi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wilaya ya Nyamagana Mhe. Witness Makale kwa ushirikiano na ofisi ya Maendeleo ya Jamii Halmshauri ya Jiji la Mwanza, Baraza la Wanawake Wilaya, Shirika la Kivulini, Desk and Chair Foundation, CRDB, SIDO, YWCA, PARALEGAL pamoja na Wanawake na Hatamu.

Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Nyamagana🇹🇿
Share To:

Post A Comment: