Tuesday, 12 March 2019

DC KASESELA : MARUFUKU WANAUME KUWAKATAZA WANAWAKE KUMILIKI ARDHI

Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela akiwa na viongozi mbalimbali wakati wa maazimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyikia katika kata ya ulanda mkoani Iringa
Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela akiwa na viongozi mbalimbali akiwa kwenye banda la mradi wa urasimishaji ardhi vijiji (LTA) ambao ndio wamesaidia kutoa hati miliki kwa wanawake na kupunguza migogoro wilaya ya Iringa
Baadhi ya wadau wakiwa kwenye banda la mradi wa urasimishaji ardhi vijiji (LTA)
 Wadu wakiwa kwenye banda la mradi wa urasimishaji ardhi vijiji (LTA)

Na Fredy Mgunda,Iringa.

WANAWAKE mkoani Iringa wametakiwa kuanza kumiliki ardhi kwa ajili ya kufanya shughuli za kimaendeleo na badala yake waachane na tamaduni kandamizi za kuwaachia wanaume katika umiliki wa mali.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Iringa Richard Kasesela katika kilele cha maadhimisho ya wanawake yaliyofanyika katika kijiji cha ibangamoyo kata ya ulanda wilaya ya Iringa alisema kuwa wanawake waaze kumiliki ardhi ili kujiinua kiuchumi kwa kuwa wanawake ndio walezi wa familia tofauti na wanaume wanaokuwa na makazi tofauti tofauti.

Kasesela aliwataka wanaume kuwapa haki wanawake kumiliki ardhi kwa kuwa wanahaki hiyo kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi hivyo mwanaume atakayemkataza mwanamke kumiliki ardhi atachukuliwa hatua za kisheria.

“Nasema nileteeni wanaume wote wanaowazuia wanawake kumiliki ardhi tutamtafutia sehemu ya kuishi kwa kuwa atakuwa anakiuka katiba ya nchi yetu hivyo ni lazima sheria ifuate mkondo wake” alisema

Akitembelea banda la mradi wa urasilmishaji ardhi vijijini (LTA), Kasesela alisema kuwa mradi huo umekuwa mkombozi kwa wanawake kumiliki ardhi kutokana na kutoa elimu kwa wanaume na kufanikisha wanawake kupatiwa hati miliki za kimila ambazo ndio limekuwa suluhisho la migogoro ya ardhi vijijini.

Aidha Mtaalam wa mawasiliano na uenezi wa mradi wa urasimishaji ardhi vijiji (LTA), Jackline Mhegi alisema kuwa katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasisitiza kuwa binadamu wote ni sawa na huzaliwa  huru hivyo basi wanatakiwa kupata ulinzi sawa na sheria za nchi ikiwepo kumiliki ardhi.

“Kwa mujibu wa ibara ya 24(I) inasema kila mtu anahaki ya kumiliki mali na haki ya hifadhi kwa mali yake aliyokuwanayo kwa mujibu wa sheria,hivyo mwanamke ana haki ya kumiliki ardhi kama mojawapo ya mali na kupata ulinzi wa mali kulingana na katiba ya nchi” alisema Mhegi

Mhegi alisema, sera ya taifa ya ardhi ya mwaka 1995 inaeleza kuwa “ni haki ya kila mwanamke kupata,kumiliki,kutumia na kuuza au kugawa ardhi  kwa kuwa hata mwanaume ana haki hiyo” Sheria ya ardhi namba 4 na 5 ya mwaka 1999,Kwa mujibu wa kifungu cha 3 (2) cha Sheria ya ardhi Na.5 ya Vijiji ya mwaka 1999 inasema “Haki ya kila mwanamke kupata, kumiliki, kutumia na kuuza au kuigawa ardhi ifahamike kuwa ni sawa na haki ya mwanamume yeyote kwa viwango vilevile na masharti yaleyale”

“Sheria hizi zimeondoa ubaguzi dhidi ya mwanamke. Mwanamke anaehitaji ardhi atafuata taratibu zinazohusika na hapaswi kunyimwa ardhi kwa sababu tu yeye ni mwanamke, Sheria ya mahakama za utatuzi wa migogoro namba 2 ya mwaka 2002, Sheria ya marekebisho ya utatuzi wa migogoro namba 2 ya mwaka 2004, Sheria ya ndoa ya mwaka 1971”alisema Mhegi

Mhegi alimalizia kwa kusema, Wanawake ni watumiaji wakuu wa ardhi hivyo vyombo vinavyohusika na masuala ya usimamizi na utawala wa ardhi vihakikishe kuwa wanawake na wanaume wanashirikishwa ipasavyo katika masuala yahusuyo ardhi ili kuleta usawa wa kijinsia katika usimamizi na umiliki wa ardhi utakao changia maendeleo endelevu kutoka na rasilimali ardhi kiuzalishaji, Hivyo wanawake wahakikishe wanatumia nafasi walizonanzo kwa kushiriki na kutoa mawazo yao kwa lengo la kuboresha maslahi ya familia zao na taifa kwa ujumla.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Stella Mosha, alisema ni wakati sasa kwa wanawake kutambua ya kwamba wana haki ya kumilki ardhi sawa kama wanavyomiliki wanaume kwa njia mbalimbali zikiwemo wao binafsi, wao Pamoja na waume au ndugu zao.

“Pia jamii inakumbushwa kuachana na mila na desturi kandamizi katika zinazo wazuia wanawake kuto miliki ardhi kwa sababu wakati umebadilika wanawake na wanaume wanatakiwa kushirikiana ili kuweza kuinua uchumi wa familia na baadae taifa kwa ujumla” alisema mosha

Mosha aliesma,Mradi uliweza kutoa elimu ya juu ya haki ya wanawake kupitia mikutano ya hadhara kwa kila kijiji kwa wanawake pekee na baadae kuwaunganisha na wanaume ili kuwa na majadiliano ya pamoja.

“Mradi ulitoa mafunzo juu ya Sera na Sheria za ardhi zinazoelezea haki ya wanawake kumiliki rasilimali ardhi” alisema mosha

Mosha alimalizia kwa kusema,mradi uliwajengea uwezo wanawake kuingia katika vyombo mbalimbali vinavyosimamia masuala ya usimamizi wa ardhi ngazi ya kijiji, kama vile: kamati ya Mpango bora wa Matumizi ya ardhi, Kamati ya Uhakiki wa maslahi ya ardhi, Baraza la utatuzi wa migogoro ya ardhi ya kijiji.

No comments:

Post a Comment