Monday, 20 August 2018

Tingo Ajeruhiwa Magari 7 Yakiteketea kwa moto

Idadi ya magari yaliyoteketea kwa moto katika kituo cha forodha Rusumo Wilaya ya Ngara mkoani Kagera mpakani mwa Tanzania na Rwanda, imeongezeka na kufikia saba na trekta moja huku utingo wa moja ya gari hayo akipelekwa hospitalini baada ya kujeruhiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Luteni Kanali Michael Mntenjele amesema tukio limetokea leo Agosti 19, 2018.

Kanali Mtenjele amesema utingo wa gari lililokuwa limebeba petroli alibahatika kuruka na kuumia na amepelekwa Hospitali ya Nyamiaga kwa matibabu, huku eneo la tukio likiwa limetanda taharuki kutokana na ukosefu wa gari la zimamoto.

"Tumewasiliana na viongozi wenzetu wa nchi jirani ya Rwanda wameahidi kutuma helikopta ya kuzima moto na kuokoa mali za wananchi na maisha yao," amesema.

Amesema kukosekana kwa gari la zimamoto wilayani Ngara hasa kata hiyo ya Rusumo ni changamoto kubwa katika kuokoa maisha ya wananchi na mali zao.

No comments:

Post a comment