Aliyekuwa mmiliki wa IPTL Harbinder Singh Sethi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa ana miezi 6 hajaonana na mke wake.

Mbali ya Sethi mshtakiwa mwingine ni mfanyabishara James Rugemarila ambapo wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, kutakatisha fedha na kuisababisha serikali hasara ya USD 22, 198,544.60 na Sh.Bilioni 309,461,300,158

Sethi ambaye yupo katika gereza la Ukonga ameyaeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi baada ya Wakili wa serikali Mwanaamina Kombakono kueleza kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya Wakili Kombakono kueleza hayo, Wakili wa Sethi, Dorah Mallaba aliieleza mahakama kuwa bado hawajapata kibali kwa ajili ya mshtakiwa Sethi kuonana na mkewe. Hata hivyo Wakili Mallaba aliiomba mahakama iruhusu hata kwa dakika 5 Sethi aonane na mkewe.

“Naomba mahakama itumie busara kwa kuwa mke wake yupo hapa mahakamani, aweze kuonana naye hata kwa dakika 5,”ameomba.

Wakili Kombakono baada ya kusikiliza hoja ya wakili Mallaba, alieleza kuwa kuna taratibu za kumuona mahabusu hivyo zifuatwe.

Kutokana na maombi hayo Hakimu Shahidi amesema taratibu za kuwatunza mahabusu zipo chini ya Magareza kama kuna jambo lolote mahususi basi lifikishwe mahakani, ambapo ameahirisha kesi hiyo hadi September 13,2018.

Katika kesi hiyo Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kighushi,  kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu,  kutakatisha fedha  na kuisababisha hasara ya USD 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: