Jeshi la Polisi mkoani Manyara limemuachia kwa dhamana dereva wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla, Juma Salehe (59) na kumtaka kuripoti polisi kila anapohitajika hadi uchunguzi wa ajali utakapokamilika.

Salehe alikuwa akiendesha gari la waziri huyo lililopata ajali Agosti 4, 2018 eneo la Magugu mkoani Manyara na kusababisha kifo cha aliyekuwa ofisa habari wa wizara hiyo, Hamza Temba huku wengine waliokuwemo katika gari hiyo wakipata majeraha sehemu mbalimbali mwilini, akiwemo Dkt. Kigwangalla aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Akizungumza na www.eatv.tv Kamanda wa polisi mkoani humo, Augustine Senga amesema kuwa chunguzi ukikamilika faili litapelekwa kwa mwanasheria wa serikali kwa taratibu nyingine za kisheria.

“Mtuhumiwa ataendelea kuwa chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi, tumemuachia huru kwa dhamana kwakuwa amekamilisha taratibu zote za dhamana, na atakapohitajika ataripoti Polisi wakati wowote”, amesema Kamanda Senga.

Senga amesema chanzo cha ajali hiyo iliyohusisha watu sita waliokuwa wakisafiri kutoka Arusha kwenda Dodoma ni twiga aliyekatiza barabara ghafla na dereva wa gari katika jitihada za kumkwepa liliyumba kushoto na kulia kisha likapinduka.

Kwenye ajali hiyo katibu wa Dkt. Kigwangalla, Ephraim Mwangombe (47) na Salehe ambaye ndiye aliyekuwa akiendesha gari hilo hawakupata jeraha lolote.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: