Monday, 6 August 2018

Kikwete ataka teknolojia mpya ya Kilimo


Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ametaka teknolojia mpya ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi inayooneshwa kipindi cha Maonesho ya maadhimisho ya Wakulima na Wafugaji maarufu kama Nanenane iwafikie wananchi ili kuwakwamua katika dimbwi la Umasikini.

Dkt. Jakaya Kikwete ametoa kauli hiyo Agosti 5 mwaka huu baada ya kutembelea vipando na mabanda ya maonesho ya Wakulima, wafugaji na wavuvi kwenye maonesho ya nanenane kanda ya Mashariki yanayoendelea katika uwanja wa Mwl. J. K. Nyerere mjini Morogoro.

Dkt. Kikwete amesema pamoja na wataalamu wa Sekta ya Kilimo, ufugaji na uvuvi kujitahidi kuvumbua teknolojia mpya katika Sekta hiyo bado teknolojia hiyo haiwafikii wananchi wa Vijijini hivyo amewataka pamoja na kuongeza jitihada za kuvumbua muhimu elimu hiyo waipeleke kwa wananchi ili kuondoa umaskini miongoni mwao.

“kazi kubwa imefanyika ya utafiti, viwango vimeongezeka sana vya Ubora, suala kubwa ni namnagani uvumbuzi unaofanywa na maabara kwenye vituo vyetu namna ya kuwafikia wakulima” alisema Dkt. Kikwete.

Aidha, Rais huyo mstaafu wa awamu ya Nne amesema ili kuondokana na umaskini kwa haraka wataalamu lwanatakiwa kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji namna ya kulima na kufuga kibiashara na kuondokana dhana ya kufanya kazi hizo kwa ajili ya kujikimu peke yake.

Maonesho hayo ya 25 ya nanenane kanda ya Mashariki yanayofanyika katika Uwanja wa Mwl. J. K. Nyerere katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro yanajumuisha Mikoa minne ya Pwani, Tanga, Dar es Salaam na wenyeji Morogoro.

No comments:

Post a comment