Tuesday, 14 August 2018

DC Muro atoa maagizo haya kwa madiwani


MKUU WA WILAYA YA ARUMERU, JERRY MURO.

MKUU wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro ameanza kazi kwa kutoa agizo kwa madiwani wa Halmashauri ya Arusha  vijijini kushirikiana na Mkurugenzi  wa Halmashauri hiyo, kuwasimamia watendaji na wataalamu katika ukusanyaji wa mapato ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi.

Agizo hilo alilitoa mwishoni mwa wiki katika kikao cha Baraza la Madiwani na kwamba amebaini kuwapo kwa uzembe, ukiukwaji na udanganyifu katika suala zima la ukusanyaji wa mapato kwenye Halmashauri za Wilaya ya Arumeru.

“Nilipopata fursa ya kuzungumza na watumishi niliwataka watimize wajibu wao na kabla ya kuzungumza na madiwani kwenye baraza hili, nilipita mitaani kwenye maduka machache kukagua na  kuangalia mzunguko wa biashara unavyokwenda na nilikuta leseni nyingi ni feki,”alisema.

Alisema kuwa tofauti na kukamata leseni hizo wafanyabiashara hao, hawakuwa wamelipa kodi kwa kipindi cha miaka miwili na walikuwa wakiendelea na biashara zao kama kawaida kwa muda wote bila ya watumishi wa halmashauri kubaini ukiukwaji wa kulipa kodi.

“Watumishi wa serikali wamekuwa wakinunua vitu kwenye maduka hayo, lakini hakuna hata mmoja aliyekuwa na wazo la kuuliza au kuangalia leseni ya biashara,”alisema na kuongeza:

“Wapo maofisa biashara wanadhani wajibu wao ni kutoa leseni, kukaa ofisini na kusubiri kupewa taarifa bila ya kutambua wajibu wao, wakati wanatakiwa   kwenda kufanya ukaguzi mitaani,”alisema.

Aidha, alisema endapo watumishi wa serikali watasimamia vizuri suala la ukusunyaji wa mapato, itawasaidia kusukuma gurudumu la maendeleo

kwa kutoa huduma bora kwa wananchi hususani maeneo ya vijijini.

Amelitaka baraza hilo, kuongozwa kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Noah Lembris alisema, baraza hilo limekuwa likifanya kazi kwa mujibu wa sheria na wanafanya kazi kwa kushirikiana na serikali kuu.

“Nikuhakikishie Mkuu wa Wilaya ushirikiano utakuwa zaidi ya asilimia 100 na baraza letu linafanya kazi kwa karibu na serikali kuu,”alisema.

Alisema dira ya halmashauri hiyo ni kutanguliza maslahi ya wananchi na kuhakikisha wanatoa na kupeleka maendeleo kama ilivyokuwa dhamira ya serikali.

No comments:

Post a Comment