Watoa huduma za afya wametakiwa kuhakikisha wanawafikia wadau wote muhimu ili kufanikisha zoezi la umezeshaji wa kinga tiba dhidi ya ugonjwa wa minyoo na kichocho


Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Ilemela Mheshimiwa Dkt Severine Lalila wakati wa kikao kazi cha maandalizi ya uzinduzi wa zoezi la umezeshaji kinga tiba ya kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele yakiwemo Kichocho, Minyoo, Trakoma, Usubi, Matende na Mabusha ambapo amewataka watoa huduma za afya kuhakikisha wanawafikia wadau wote muhimu ili kufanikisha zoezi hilo ili kufikia walengwa wote wa mpango huo

Wakati wa kuendesha zoezi hili la uhamasishaji niwaombe muwafikie wadau wote ambao pengine mnadhani wakati uliopita hamkuwafikia, tukifanikiwa kuwafikia hao itakuwa ni juhudi ya sehemu ya kulinda afya za waTanzania …’ Alisema


Aidha Mheshimiwa Dkt Lalila mbali na kuwaasa wataalamu wa afya kuwa wabunifu ili kulinda afya za wananchi, ameishukuru Serikali kwa kuanzisha mpango huo wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele huku akiitaka jamii na wadau wengine kuunga mkono jitihada hizo za Serikali.

Kwa upande wake mratibu wa mpango huo kwa manispaa ya Ilemela, Bi Gisela Urasa amesema kuwa  zoezi la umezeshaji tiba kinga ya magonjwa ya Kichocho na Minyoo kwa watoto walio mashuleni wenye umri wa kuanzia miaka 5 hadi 14 linataraji kufanywa siku ya jumatatu Agosti 6 na 7 kwa watakaokosa siku ya kwanza huku ikijumuisha idadi ya wanafunzi 96,102 kwa shule 116 zinazopatikana ndani ya wilaya hiyo


Nae mganga mkuu wa wilaya ya Ilemela Dkt Florian Tinuga amekemea upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya watu wenye nia ovu na zoezi hilo juu ya kuwepo kwa madhara ya kiafya yanayotokana na umezaji wa tiba kinga hiyo nakusisitiza kuwa Serikali haitavumilia mtu yeyote atakaekwamisha zoezi hilo  kwa kumchukulia hatua kali za kisheria  pamoja na kuwaomba wazazi kutoa ushirikiano kwa kuwafikisha watoto kwenye vituo vilivyopangwa vya kutolea huduma hiyo na kuwapa chakula watoto hao masaa mawili kabla ya kumeza dawa.


Kikao kazi hicho cha uendeshaji wa zoezi la umezeshaji tiba kinga kilihusisha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya Ilemela, madiwani wa kata zote 19 za manispaa hiyo na watendaji wa  kata kwa wakati tofauti tofauti ili kuhimiza ushirikiano na wajibu wa kila mmoja katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: