Jeshi la Polisi mkoani Singida linamshikilia Jamal Makere (37) mkazi wa Utemini mjini Singida kwa tuhuma za kumuua mgoni wake, Ramadhan Athuman (27) anayedaiwa kwenda nyumbani kwa mtuhumiwa kwa lengo la kumfuata mkewe kimapenzi.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike alisema tukio hilo ni la juzi kuamkia jana saa 6.00 usiku.

 Inadaiwa kijana Ramadhan akiamini Jamal hayupo nyumbani kwake, alienda kugonga mlango kwa lengo la kutaka kufanya mapenzi na mke wa Jamal, kwani ilikuwa ni mazoea yao kukutana usiku kwa ajili ya kuhondomola tendo la ndoa 'kufanya mapenzi'.

Hata hivyo, kutokana na usemi “Siku za mwizi ni arobaini,” siku hiyo mwenye nyumba alikuwepo na Ramadhan alipogonga mlango Jamal alitoka haraka, akamkuta ‘mwizi’ wake bado anamsubiri hawara (jina limehifadhiwa) kisha wakaanza kupigana hatimaye Ramadhan alielemewa. Kamanda Njewike alisema Ramadhan aliumizwa vibaya na kipigo hicho hivyo alikimbizwa hospitalini.

Hata hivyo juhudi za madaktari, hazikufua dafu na hatimaye aliaga dunia. Uchunguzi wa awali wa Polisi ulibaini kuwa mtu huyo alikuwa na mahusiano na mke wa mtuhumiwa na walikuwa na mazoea ya kukutana mara kwa mara nje ya nyumba ya mtuhumiwa. 

Hili ni tukio la pili katika siku zisizozidi tano mkoani hapa, linalotokana na masuala ya mapenzi. 

Agosti 15 mwaka huu, wanandoa wawili walipoteza maisha yao katika tukio lililohusishwa na wivu wa mapenzi.
Share To:

Anonymous

Post A Comment: