Tuesday, 10 July 2018

Vigogo Watano KNCU , TCCCO Kizimbani kwa Uhujumu Uchumi

Viongozi watano wa Chama cha Ushirika mkoa wa Kilimanjaro(KNCU LTD) na Kiwanda cha Kukoboa Kahawa cha Tanganyika (TCCCO) jana wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ,Moshi na kusomewa Mashtaka tofauti yakiwemo ya uhujumu Uchumi.

Waliofikishwa Mahakamani na kupandishwa Kizimbani ni pamoja na Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Kikuu cha Ushirika ,Kilimanjaro (KNCU) Aloisi Kitau (70) Makamu Mwenyekiti mstaafu wa KNCU,Hatibu Mwanga(70) na Meneja Mkuu wa KNCU ,Honest Temba (38).

Wengine waliofikishwa mahamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi ,Pamela Mazengo ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Kukoboa Kahawa (TCCC0) Maynard Swai (57) na aliyekuwa Meneja Mkuu wa TCCCo ,Andrew Kleruu wanaotajwa kukiuka sheria wakati wa ununuzi wa mtambo wa kukoboa Kahawa.

 
Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi jana saa nne asubuhi wakiwa chini ya ulinzi polisi.

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka na wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavulla saa 6:25 mchana.

Wakili Chavulla akishirikiana na mawakili wa Serikali, Jackline Nyantori na Shiza Kimera aliiarifu mahakama kuwa upelelezi wa kesi haujakamilika. Hakimu aliiahirisha hadi Julai 24.

Chavulla akiwasomea mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Pamela Mazengo alidai kati ya Julai 2014 na Novemba 2017, Kitau, Mwanga na Hatibu walitumia vibaya madaraka wakiwa viongozi wa KNCU.

Alidai katika tarehe tofauti, washtakiwa waliilipa kampuni ya Oceanic Link Shipping Services fidia ya Sh2.9 bilioni kitendo kilichoinyima haki KNCU.

Kampuni hiyo ilikuwa imewekeza katika shamba la Garagagua lenye ukubwa wa ekari 3,429. KNCU ililiuza shamba hilo kwa Sh9.3 bilioni ili kulipa madeni ukiwamo mkopo wa Benki ya CRDB.

Katika shtaka la pili, Chavulla alidai katika kipindi hicho, washtakiwa kwa kukusudia waliilipa kampuni hiyo na kuisababishia KNCU hasara ya Sh2.9 bilioni.

Katika kesi inayowakabili Swai na Kleruu, wanadaiwa kati ya Januari 2014 na Desemba 2015 walitumia vibaya madaraka yao na kununua mtambo wa kukoboa kahawa bila kufuata utaratibu.

Chavulla alidai washtakiwa hao walinunua mtambo wa kukoboa kahawa kutoka kampuni ya Brazafric ya Brazil bila kufuata utaratibu na kuisababishia TCCCo hasara ya Sh1.67 bilioni.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mashtaka yanayowakabili husikilizwa na Mahakama Kuu. Washtakiwa hao walipelekwa rumande kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka kisheria ya kusikiliza shauri hilo na upelelezi wa kesi hizo haujakamilika.

No comments:

Post a Comment