Watumishi wa Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA) wameshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Shekh Amri Abeid Jijini Arusha.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango amewapongeza wafanyakazi wote nchini wakiongozwa na TUCTA kwa kazi kubwa wanayoifanya inayopelekea maendeleo katika sekta mbalimbali na kuwanufaisha wananchi kwa ujumla.

Dkt. Mpango amesema serikali inatambua umuhimu wa motisha ambazo zitaleta tija katika uboreshwaji wa maslai ya wafanyakazi, hivyo kupitia uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan suala hilo litafanyiwa kazi, huku akiwaasa wafanyakazi ambao hawatimizi majukumu yao wajitafakari na kuhakikisha wanabadilika na kuongeza juhudi katika kazi zao.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema siku ya wafanyakazi hutoa fursa ya kufanya tasmini ya kazi zilizofanyika na kuweka mipango na mikakati mipya ya siku za mbeleni ili kuhakikisha wafanyakazi wanakuwa chanzo cha mapinduzi makubwa ya kimaendeleo hapa nchini.

Waziri Mkuu ameahidi kuwa Ofisi yake itakuwa bega kwa bega na wafanyakazi wote katika kutekeleza majukumu yao ili kuhakikisha serikali na wananchi kwa ujumla wanafikia malengo yake hasa katika mapinduzi makubwa ya kiuchumi.

Mgeni rasmi katika Maadhimisho haya kitaifa alikuwa Makamu wa Rais Mhe. Philip Isdor Mpango, huku Kauli Mbiu ya mwaka huu ikiwa ni “Nyongeza ya Mishahara ni Msingi wa Mafao Bora na Kinga Dhidi ya Hali Ngumu ya Maisha”.



Share To:

Post A Comment: