Saturday, 7 July 2018

TCRA yaagizwa kuzishughulikia kampuni za ving’amuzi

Mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA) imetakiwa kuzichukulia hatua kampuni za ving'amuzi ambazo zinakiuka leseni kwa kuzuia matangazo ya chaneli za bure.

Agizo hilo limetolewa jana Julai 6 na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi   Mhandisi Atashasta Nditiye wakati kamati ya bunge ya miundombinu ilipotembelea (TCRA).

Mhandisi Nditiye amesema serikali haitazifumbia macho kampuni zinazoleta michezo ya kijanja wakati zinafahamu fika maelekezo ya leseni zao.

"Hakuna kufumbia macho, kama kuna mtu nyumbani kwake hajalipia king'amuzi halafu amekatiwa chaneli za bure asisite atoe taarifa na hatua zichukuliwe haraka,"

Amesema kampuni za Star times, Digitek, Ting na Continental zinatakiwa kurusha bure chaneli tano za hapa nchini ili kuwapa fursa wananchi kupata taarifa. Chaneli hizo ni TBC, ITV, Channel ten, EATV na Star TV.

Nditiye pia ameziagiza kampuni za simu kuzingatia usajili wa laini kwa kutumia teknolojia ya biometriki ambayo inahusisha uchukuaji wa alama za vidole na picha ya mtumiaji wa namba husika.

Amesema mfumo huo wa usajili una lengo la kuhakikisha namba moja ya simu inatumiwa na mtu mmoja hivyo itasaidia kukabiliana na vitendo vya matumizi mabaya ya mawasiliano.

"Niwaambie watanzania kuwa changamoto ya watu kutumia vibaya laini za simu limeshapatiwa ufumbuzi na linakwenda kumalizika kabisa muda si mrefu kutokana na mfumo huu,”

“Sasa mtu akisajili namba lazima zichukuliwe alama za vidole na picha apigwe ili tujue kabisa namba fulani inatumiwa na nani,”

Kuhusu utapeli unaofanywa na wanaotuma meseji za kuelekeza fedha itumwe amesema tatizo hilo limeshatatuliwa.

No comments:

Post a Comment