Kampuni ya Udalali ya MEM imetangaza kuyauza mabasi 47 ya Kampuni ya Mohamed Trans, baada ya mmiliki wake kushindwa kurejesha mikopo anayodaiwa.
 
Mkugenzi wa Kampuni ya MEM, Eliezer Mbwambo, alisema mabasi hayo yatanadiwa kwenye mnada wa hadhara Julai 21 na 28, mwaka huu, mkoani Shinyanga.

Alisema mbali na mabasi hayo, pia watauza viwanja na nyumba ambavyo vinamilikiwa na mfanyabiashara huyo.

“Kwa idhini tuliyopewa na Nzaro Nuhu Kachenje ambaye ni msimamizi wa Kampuni ya Mohamedi Trans Ltd, tutauza kwa mnada wa hadhara mabasi na nyumba. Mnada utafanyika sehemu nyumba na mabasi yalipo,” alisema Mbwambo.

“Mabasi 47 yako kwenye yadi ya Mohamed Trans Shinyanga na basi moja liko kwenye yadi ya MEM Mikocheni wakati kiwanja na nyumba viko kwenye kiwanja kimoja Nyegezi jijini Mwanza,” alisema.

Alitaja vingine vitakavyouzwa kuwa ni pamoja na viwanja na nyumba vilivyoko kwenye kiwanja namba 557 eneo la Ngokolo, Shinyanga.

Mmoja wa wafanyabiashara wa mabasi ambaye hakutaka jina lake litajwe  alisema biashara yao imeyumba na hali hiyo huenda itawakuta wamiliki wengi wa mabasi.

“Watu wanaweza kudhani sisi wafanyabiashara wa mabasi tunapata sana lakini hali haiko hivyo. Watu wengi wana mikopo wanashindwa kuirejesha. Ni suala la muda tu, wengi tutafika huko alikofikia mwenzetu,” alisema.

Aidha, alisema biashara hiyo ni ngumu kwa sababu mmiliki analazimika kuagiza mabasi mapya na ya kisasa kila baada ya muda ili kujihakikishia kuwa na wateja wa kudumu muda wote.

“Huyu mwenzetu mabasi yake ni yale yale ya miaka yote. Sasa watu wameshaingiza matoleo mapya mengi tu, nani atapanda Marcopolo la miaka hiyo? Hii biashara si ya kuingia kichwa kichwa unaweza kushindwa kulipa mikopo,” alisema mtoa habari huyo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: