Friday, 13 July 2018

Kauli ya Babu Tale kuhusu Mavoko Kutimuliwa WCB

 BAADA ya kuzagaa kwa madai kwamba msanii wa Bongo Fleva, Rich Mavoko ambaye yuko kwenye Kundi la WCB ambalo mkurugenzi wake ni mwanamuziki, Nasibu Abdul ‘Diamond’ kuwa ametimuliwa kwenye kundi hilo, meneja wao Hamis Taletale ‘Babu Tale’ ameibuka na kufunguka ukweli.

Akizungumza na Ijumaa kwa njia ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp akiwa Marekani, Babu Tale alisema kwamba tetesi hizo siyo za kweli na Mavoko bado yupo WCB ila kipindi ambacho walikuwa wanachukua video ya Reality Show aliyoiposti Diamond ambayo ndiyo iliyozua maneno mwanamuziki huyo hakuwepo alikuwa kwao Mahenge, Morogoro kwenye msiba kwani alifiwa na dada yake.


“Wakati tunarekodi hiyo video ya Reality Show, Mavoko alikuwa Mahenge kwao, alifiwa na dada yake kwa hiyo alikuwa kwenye msiba, lakini hizi siku zote yupo bize anashuti wimbo wake mpya na zamu inayokuja ni yake kuachia wimbo kwani sisi huwa tunaachiana muda wa kutoa nyimbo kwa hiyo sioni haja ya kuongopa kwamba hayupo WCB, kwa sababu hata asipokuwepo lazima itajulikana tu,” alisema Babu Tale.

Ili kuujua ukweli zaidi kuhusiana na suala hilo, Ijumaa lilimtafuta Mavoko mwenyewe ambapo alisema hayo ni mambo ya ajabu sana kwake hivyo hawezi kuongea chochote labda utafutwe uongozi wa WCB wenyewe ndio uzungumze.

“Siwezi kuongea mambo hayo, mambo ya ajabu sana hayo naombeni muutafute uongozi wa WCB wenyewe labda ndiyo utazungumza,” alisema Mavoko.

No comments:

Post a Comment