Na. Jeshi la Polisi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro amewasili mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi na anatarajiwa kufunga mafunzo katika Chuo cha Polisi Wanamaji Mwanza ambayo yana lengo la kukabiliana na uhalifu unaotokea katika Bahari, Maziwa na Mito hapa nchini.

Pamoja na ufungaji wa mafunzo hayo pia ataendelea na ziara ya kukagua utendaji wa Polisi katika baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa lengo la kuhakikisha uhalifu unapungua  hapa nchini ikiwemo ajali za barabarani, Maujai ya kishirikina na uhalifu katika Visiwa vilivyopo Ziwa Viktoria.

Mapema baada ya kuwasili amezungumza na Maofisa wa Polisi waliopo Mkoani Mwanza na kusisitiza kufanya kazi kwa weledi pamoja na kuhakikisha kuwa ajali zinapungua katika maeneo yao.

“Nimekuja kukagua utendaji wenu ili kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili ili kufikia malengo tuliyojiwekea ya kuhakikisha uhalifu unapungua hapa nchini, hivyo ni imani yangu kila mmoja atawajibika kwa nafasi yake na kuwasimamia waliopo chini yake ipasavyo” Alisema IGP Sirro

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi DCP Ahmed Msangi amesema hali ya usalama katika mkoa huo ni shwari na suala la usalama barabarani linaendelea kusimamiwa kikamilifu kwa kushirikiana Mamlaka nyingine zinazohusika.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: