Friday, 1 June 2018

Serikali kutoa ajira za moja kwa moja kwa Wanafunzi


Serikali imesema inaandaa utaratibu maalumu wa kutoa ajira za moja kwa moja kwa wanafunzi wa fani mbalimbali za ufundi kutoka vyuoni ili kuepusha usumbufu wanaopata katika kutafuta ajira mara baada ya kuhitimu masomo yao.

Hayo yamesemwa leo Juni 1, 2018 Bungeni, Jijii Dodoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, na Walemavu, Anthony Mavunde na kuongeza kuwa serikali itawaunganisha moja kwa moja wahitimu hao pamoja na wadau mbalimbali nchini ambao hutoa nafasi za ajira katika fani za ufundi.

“Tunachokifanya kama Serikali kwanza kabisa kwa kushirikiana na Sekta binafsi ambapo pindi nafasi zinapopatikana huwa tunaunganisha moja kwa moja na vyuo vyetu vya ufundi ili vijana hawa waweze kupata nafasi za ajira za moja kwa moja, sisi kama Serikali tutaona namna ya kuunganisha vyuo vyetu vya ufundi pamoja na waajiri nao wapate nafasi za moja kwa moja” amesema Mavunde

Mavunde ameongeza kuwa serikali itatumia mfano wa baadhi wa vyuo vya ufundi kikiwemo chuo cha Don Bosco ambacho hufanya kongamano wadau wa fani za ufundi ili kuweza kutoa fursa za ajira kwa vijana wanohitimu katika chuo hicho.

Kwa upande mwingine Naibu Waziri huyo amedai kuwa Serikali imeweka vituo vya kulea vijana ambavyo ni Sasanda (Mbeya), Ilonga (Morogoro) na Kilimanjaro lengo likiwa ni kuandaa vijana kuwa na sifa za kuajirika na pia Serikali imetenga mfuko wa maendeleo ya vijana ili kutoa mikopo kwa vijana.

No comments:

Post a comment