Monday, 21 May 2018

OKWI ADAI HATAMSAHAU KASEJA MAISHANI


MSHAMBULIAJI wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi, amesema kuwa licha ya timu hiyo kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara, kamwe hawezi kumsahau kipa wa Kagera Sugar, Juma Kaseja kwa kitendo chake alichomfanyia juzi Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, Dar.

Juzi Jumamosi, Kaseja alidaka penalti ya Okwi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara na kuiwezesha timu yake ya Kagera Sugar kuvunja rekodi ya Simba ambayo ilikuwa ikiishikilia ya kutofun­gwa katika ligi hiyo msimu huu.

Katika mchezo huo ambao ulikuwa ni wa mwisho wa Simba katika uwanja wake wa nyumbani na ambao pia ulishuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli, Simba ilifungwa bao 1-0.

Akizungumza na Championi Ju­matatu, Okwi alisema kuwa kamwe hatamsahau Kaseja kwa kitendo hicho alichomfanyia mbele ya rais.

“Alifanya nijisikie vibaya sana licha ya kwamba tulikuwa tukikabidhiwa pia kombe la ubingwa wa ligi kuu, kusema kweli sitamsahau.

“Sikuwahi kukosa penalti msimu huu ila Kaseja kasababisha niandike rekodi hiyo lakini nampongeza kwa uwezo mkubwa aliouonyesha na ku­fanikiwa kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi,” alisema Okwi ambaye ndiye kinara wa kuzifumania nyavu mpaka sasa akiwa na mabao 20.

No comments:

Post a comment