Mbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya CHADEMA, Mchungaji Peter Msigwa amefunguka na kuwakaribisha wageni wote katika kusherehekea siku ya Mei Mosi ambayo kitaifa inafanyika mkoani Iringa leo na kuwaomba wanachama na wafuasi wa UKAWA wasivae jezi zozote zile uwanjani.

Msigwa amesema hayo leo Mei 1, 2018 na kusema kuwa watu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameichukulia siku hiyo ya wafanyakazi dunia kufanya siasa na kusema wameng'oa bendera za CHADEMA na kuweka bendera za CCM hata kwenye nguzo za umeme kinyume na utaratibu.

"Wenzetu wanatumia sherehe hizi kisiasa kwa kung'oa bendera za CHADEMA na kuweka bendera za CCM hata kwenye nguzo za umeme! Kinyume cha utaratibu, Utadhani ni sherehe ya kuzaliwa kwa CCM. Mji ungepambwa kwa bendera za taifa ingeleta mshikamano na umoja wa Taifa. Kwa bahati mbaya wameashindwa kuona hili. Hata hivyo niwaase wapenzi na wanachama wa CHADEMA na UKAWA! Wasije uwanjani na nembo au bendera za vyama. Tuonyeshe ukomavu na uelewa wa kisiasa" alisema Msigwa

Aidha Mbunge Msigwa amewaomba watu wa Iringa waweze kuwapokea na kuwakarimu vizuri wageni hao ili watamani kurudi tena Iringa ili wakuze uchumi wa Manispaaa hiyo ya Iringa.

Mbali na hilo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ndiye mgeni rasmi katika sherehe hizo hivyo anatarajiwa kuhotubia taifa kutokea Iringa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: